Alliance, African Lyon ni vita ya kisasi Ligi Kuu

Wednesday January 9 2019

 

By Masoud Masasi

ALLIANCE FC kwa sasa iko Dar es Salaam huku benchi la ufundi la timu hiyo likisema  watahakikisha wananyakuwa pointi tatu katika mchezo wao na African Lyon utakaopigwa kwenye uwanja wa Uhuru.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa kwenye uwanja wa Kirumba jijini Mwanza timu hizo zilitoka sare ya 1-1 huku  Alliance walisawazisha jioni kwa bao la Michael Chinedu.

Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Malale Hamsini alisema anajua mchezo huo utakuwa mgumu lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi.

“Tunahitaji pointi tatu katika huu mchezo najua utakuwa mgumu kwani wapinzani wetu hawapo kwenye nafasi nzuri kwa sasa kwenye msimamo wa Ligi hivyo tutaingia kwa tahadhari kubwa,” alisema Hamsini.

Alisema kwa sasa anajivunia umairi wa safu yake ya ulinzi ambayo katika mechi tatu walizocheza imekuwa bora sana tofauti na mwanzo kwenye mchezo wao na Kagera Sugar.

“Kulikuwa na shida katika safu ya ulinzi lakini sasa nimeona imeimarika sana kwenye mechi yetu na Mbao FC walicheza vizuri sana hili limenipa nguvu sana”alisema Kocha huyo.

Mpaka sasa Alliance FC wana pointi 21 huku wakiwa katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ambao unaongozwa na Yanga wenye alama 50.

 

Advertisement