Aliyewatungua Simba sasa mambo magumu FDL

Muktasari:

Salehe alisema tayari amecheza mechi tatu baada ya kutolewa na Simba, ila katika michezo hiyo amefunga bao moja pekee - tena kwa mbinde tofauti na mwanzo ambapo alikuwa hapati upinzani mkubwa.

STRAIKA wa Stand United, Miraji Salehe amesema amegundua kuwa tangu afunge bao katika mchezo wao na Simba wa Kombe la FA, amekuwa akipata wakati mgumu kuwatoka mabeki wa timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwani wamekuwa wakimkamia kinoma.

Salehe aling’ara katika mchezo huo wa Kombe la FA, ambapo alifunga bao la kusawazisha katika sare ya 1-1 kwenye pambano la kusaka tiketi ya kucheza robo fainali ambapo Simba walishinda kwa mikwaju ya penalti ya 3-2 mtanange uliopigwa mjini Shinyanga.

Salehe alisema kwa sasa amekuwa na wakati mgumu kila mchezo wa FDL anaocheza, kwani amekuwa akikamiwa na timu pinzani wanazokutana nazo kwenye ligi hiyo.

Alisema kabla ya kucheza na Simba alikuwa hapati tabu kwenye mechi zao, lakini baada ya kufunga bao katika mchezo huo mambo yalianza kubadilika kwa kuwa amekuwa akikutana na upinzani mkali kutoka kwa mabeki wa timu pinzani.

Salehe alisema tayari amecheza mechi tatu baada ya kutolewa na Simba, ila katika michezo hiyo amefunga bao moja pekee - tena kwa mbinde tofauti na mwanzo ambapo alikuwa hapati upinzani mkubwa.

“Tumecheza na Geita Gold, Gipco na Mashujaa baada ya kucheza na Simba, lakini hizi mechi nimekutana na upinzani mkubwa, angalia nimefunga bao moja tu ambalo nalo nilipambana sana,” alisema Salehe.

Alisema kwa sasa amefunga mabao manane ambapo katika kipindi hiki atajifua ili atakaporejea awe fiti kupambana na mabeki hao ambao wamekuwa wakimchezea kindava.