Aliyewafunga Simba amtaja Onyango

Saturday October 24 2020
onyango pic

MFUNGAJI wa bao la Prisons dhidi ya Simba, Samson Mbangula amewataja Erasto Nyoni na Joash Onyango kuwa kama sio kucheza kwa akili mbele yao, basi wangewanyima ushindi wanaotamba nao.

Mbangula alisema mabeki hao wanatumia akili ya hali ya juu kulinda lango lao na ndicho kilichomfanya asijiulize mara mbilimbili dakika ya 48 kufunga kwa kichwa.

“Yaani nimefunga bao mbele ya beki wa timu ya taifa ya Kenya ambaye ni Onyango, pia mbele ya kaka yangu Nyoni mwenye uwezo wake licha ya kwamba hajaitwa timu ya Taifa, ila ni mkongwe anayetumia akili,” alisema.

Ukiachana na bao walilopata Prisons, alikiri Simba ilikuwa inacheza kitimu muda wote, jambo ambalo ikikutana na timu ambayo inacheza kwa kujiachia ni rahisi kuvuna mabao mengi.

Naye beki wa timu hiyo, Salum Kimenya alisema mechi yao na Simba waliichukulia kama wanavyoheshimu mechi nyingine wanazocheza na kwamba, kwa sasa wanaangalia mbele na kusahau matokeo hayo.

“Kila mechi tunayocheza lazima tuheshimu wapinzani, kwa sababu tunajua wapo kwa ajili ya kuhitaji pointi tatu,” alisema.

Advertisement

Naye katibu wa timu hiyo, Ajabu Kifukwe alisema ushindi huo umeongeza morali kwa wachezaji wao, kutamani kupata pointi zaidi mechi ambazo zipo mbele yao.

Advertisement