Aliyemjeruhi Nyoni aomba msamaha

Muktasari:

  • Mohammed maarufu kama Kokoy, aliliambia Mwanaspoti kuwa tukio hilo lilitokea kwa bahati mbaya wakati wa kuuwahi mpira uliokuwa mbele ya Nyoni.

UNGUJA.UKISIKIA uungwana ndio huu, Beki wa KMKM, Hafidh Mohamed aliyemjeruhi, Erasto Nyoni kwenye pambano lao la Kombe la Mapinduzi 2019, amemuangukia na kumuomba msamaha nyota hiyo wa Simba, akidai hakukusudia kumuumiza.

Mohammed maarufu kama Kokoy, aliliambia Mwanaspoti kuwa tukio hilo lilitokea kwa bahati mbaya wakati wa kuuwahi mpira uliokuwa mbele ya Nyoni.

Alisema si jambo jema mchezaji kuumia ingawa kwenye soka huwa inatokea hivyo na anasikitika kumuweka nje ya uwanja nyota mwenzake ambaye anategemewa ndani ya Simba.

“Naomba Nyoni anisamehe sana, aelewe tu kwamba sikukusudia kumuumiza hakuna mtu anayefurahia kuumia kwa mwenzake hasa kwenye soka, imeniuma kwani nimemrudisha nyuma,” alisema Kokoye na kuongeza; “Sio Nyoni pekee anayestahili kunisamehe bali ni Wanasimba wote nawaomba msahama huo, nafahamu Nyoni ni tegemeo katika timu yao ila hii ni kama ajali, namuombea kwa Mungu amponye haraka.”

Beki huyo alimshauri kocha wa Simba, Patrick Aussems kwa kumwambia; “Simba ina wachezaji bora sana naamini kwa mtu anayefuatilia mpira anaelewa ila namshauri kocha wao mechi zijazo za Kombe la Mapinduzi asiwatumie wachezaji wake muhimu ili kuepusha majanga kama hayo yasiyotegemewa.”Kokoy aligongana na Nyoni na dakika ya 41 katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Amaan na Simba kushinda bao 1-0, huku beki huyo akishindwa kuendelea na mchezo na taarifa zinasema atakuwa nje kwa wiki tatu.