Ali apigiwa saluti

Thursday September 3 2020

By HAMISI NGOWA

UONGOZI wa Klabu ya Vanga United umepewa muda wa mwezi mmoja zaidi kuendelea kuweka mikakati ya kuiendeleza klabu hiyo licha ya kipindi cha kumaaliza muda wao.

Katika kikao kilichofanyika Jumapili na kuhudhuriwa na wanakamati wote pamoja na wakereketwa wa klabu hiyo,Mwenyekiti wa sasa Mohamed Ali pamoja na jeshi lake waliongezewa muda wa mwezi mmoja wa kuendelea kuisimamia klabu hiyo.

Taarifa za kikao hicho zilieleza uongozi wa sasa na Katibu Mbaruk Kombo pamoja na wanakamati wengine,ulipigiwa saluti kwa kazi nzuri unayoifanya kwa kuhakikisha klabu inafikia upeo wa ufanisi.

“Kikao hiki cha viongozi kimekuwa cha kutathimini maendeleo ya na tumeridhishwa na kazi inayofanywa na uongozi ulioko na hivyo tunaupa muda wa kuongoza  kwa mwezi mmoja zaidi tukiweka mikakati ya kufanya uchaguzi," akasema mmoja wa Wazee wa labu hiyo.

Kulingana na Mkufunzi wa klabu hiyo, Mohamed  Waziri uongozi ulioko umefanikisha mengi mazuri ya kupigiwa mfano ikiwemo kuisajili klabu kwa Shirikisho Kuu la Soka nchini FKF.

Uongozi huo pia unapongezwa kwa kusaidia kutengeneza timu ya chipukizi wa umri chini ya miaka 17 maarufu Vanga Utd  under 17 ambayo imekuwa mwiba sumu kwa timu pinzani za chipukizi katika eneo hilo.

Kocha huyo anasema uamuzi ulioafikiwa na Bodi  Kuu ya Klabu hiyo wa  kuupa uongozi uliopo muda zaidi wa kuongoza klabu ulikuwa wa busara na wenye nia njema kwa klabu hiyo inayojiandaa kwa msimu mpya wa Ligi ya FKF eneobunge la Lunga Lunga.
.

Advertisement