Ali Kiba, Coastal Union kimaslahi zaidi unaambiwa

Muktasari:

Unajua iko vipi? Mgunda amekiri Alikiba ni mchezaji wa Coastal Union ila kutokana na hali halisi ya kiuchumi anaanza kumtumia kwa matumizi sahihi tu.

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Coastal Union ya Tanga, Juma Mgunda ana akili balaa, sasa ameamua kumtumia supastaa wake Ali Kiba kuhakikisha timu yao inajipatia kipato na kukidhi mahitaji madogo madogo.

Unajua iko vipi? Mgunda amekiri Alikiba ni mchezaji wa Coastal Union ila kutokana na hali halisi ya kiuchumi anaanza kumtumia kwa matumizi sahihi tu.

Amesema, Ali Kiba ambaye ni msanii wa Bongo Fleva na anacheza nafsi ya ushambuliaji kuwa ni brandi, hivyo atakuwa anaangalia mechi ambazo zitawanufaisha kimchezo na kimaslahi

"Kiuchumi Ali kiba tunatamani kumtumia zaidi katika mechi za nyumbani, ila ikitokea jambo la kiushindani atatumika za mikoani lakini si ovyo ovyo,"alisema Mgunda ambaye alikuwa mchezaji wa zamani wa Coastal Union.

"Nimesema Ali kiba ni mtumishi wa Coastal Union kwa hiyo mimi ndiye najua nimtumie wapi, kuna mechi ambazo ninahitaji pointi tatu hivyo lazima acheze, lakini zipo zile ambazo tunaweza kupata pointi tatu bila yeye kucheza."