Ajibu ni kama Boban tu

IMEELEZWA kivuli cha kiungo mkongwe, Haruna Moshi ‘Boban’ kinaonekana ndani ya mguu wa Ibrahim Ajibu wa Simba, lakini bado hajakitendea haki ya kufikia uwezo wa mtangulizi wake, aliyewavutia wengi katika kazi zake.

Kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Amri Kiemba alisema kipaji kama Boban huwa kinatokea kwa nadra duniani kote, akiamini inakuwa ni zawadi kutoka kwa Mungu, hivyo kwa miaka ya hivi karibuni anaona kinazunguka kwenye miguu ya Ajibu ambaye bado hajakitendea haki.

Alisema Boban ni mchezaji wa kizazi chao, aliyekuwa anarahisisha mazingira magumu kuwa mepesi mbele ya wapinzani wao uwanjani, iwe kwenye kikosi cha Simba ama Taifa Stars, walikuwa wanamuita mtu wa mipango mahususi.

“Kipindi tunacheza vipaji vilikuwa vingi ila cha Boban kilikuwa cha aina yake, aliufanya mpira uwe rahisi, ikitokea mnamiliki mpira na wapinzani wameziba njia zote na hamjui mfanye nini, mnamtafuta alipo, mkimpasia tu, kila kitu kilikuwa kinakwenda sawa,” alisema Kiemba na aliongeza:

“Kivuli cha Boban katika ligi ya sasa kipo kwa Ajibu ambaye bado hajafikia kile alichokifanya kaka yake, ninachokiona apatikane mtu wa kumkalisha chini amueleze kwamba faida ya tunu yake ya mguu sio faida kwa Simba bali hata kwenye timu ya Taifa Stars inahitajika.”

Alisema Ajibu japokuwa hana mambo mengi uwanjani, akitolea mfano timu isipokuwa na mpira anakuwa haonekani, tofauti na wale ambao anacheza nao namba yake ndani ya Simba, lakini kipaji chake akikitendea haki anaamini atakuwa mfano wa kuigwa kwa wale wanaokuja nyuma yake.

“Kuhusu uvivu wa mazoezi sio ishu kwa sababu wachezaji wengi wenye vipaji hawafanyi mazoezi mengi sana wanakuwa wanajiamini kupitiliza, tofauti na wale ambao wanajituma ili kuziba udhaifu wao, kinachotakiwa kufanyika kwa Ajibu asaidiwe kutambua thamani yake na jinsi anavyochukuliwa kwa uzito na Watanzania,” alisema.

Kiungo wa Ruvu Shooting, Shaban Kisiga alisema bado hajaona wa kumfananisha na Boban, kwamba Ajibu atatakiwa afanye kazi kubwa ya kukifanyia haki kipaji chake.

“Kipaji cha Boban hata sisi wachezaji wenzake kinatustaajabisha, ukikaa chini ukimwangalia anavyocheza unafurahia, bado sijaona wa kumfananisha naye kabisa, jamaa anatisha.”