Ajibu anajichelewesha mwenyewe

Muktasari:

Kutokana na namna ambavyo mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu anavyoonyesha kiwango cha juu tangu msimu wa Ligi Kuu Bara ulivyoanza, beki wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Abdi Banda amemwambia ni wakati wake wa kutoka na kwenda kutafuta changamoto nyingine nje ya nchi.

MABAO nane kati ya 11 ya Yanga aliyohusika nayo hadi sasa katika Ligi Kuu Bara na bao lake tamu lililogeuka kuwa gumzo la jiji kwa sasa, limemfanya beki wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Banda kufungua kinywa akidai straika huyo anajichelewe mwenyewe.
Banda anayekipiga Baroka FC iliyopo Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL), amemtaka Ajibu aachane na soka la Bongo na kwenda kutafuta changamoto nyingine nje ya nchi kwa sababu ana kila kitu anachotakiwa kuwa nacho mchezaji wa anga hizo za kimataifa.
Banda ametamka baada ya kumwona Ajibu kiwango chake kipo juu na kwamba kwa Tanzania ameshamaliza kila kitu.
Beki huyo wa Taifa Stars, alisema ameguswa kutokana namna Ajibu anavyofanya vizuri na hasa alivyoanza kwa kasi katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
Ajibu ametengeneza nafasi sita za mabao ya Yanga sambamba na kufunga mawili kati ya 11, waliyonayo mpaka sasa.
Bao hilo la 11, la Yanga alilipachika mwenyewe na kufanya awe gumzo midomoni mwa wadau wa soka Tanzania kutokana na uhodari aliouonyesha.
Alilifunga akiwa umbali wa zaidi ya 20 kutoka langoni mwa Mbao FC na kubinjuka 'tiktak' kuiandikisha timu yake la pili la la ushindi katika mechi ya Ligi Kuu Bara uliopigwa Taifa.
"Kitu kikubwa ambacho naweza kumwambia Ajibu kwa sasa, nadhani muda wake wa kucheza nyumbani umekwisha kwani kila kitu ameshamaliza na sasa atafute changamoto nyingine nje ya Tanzania bila kujali ni Ulaya au sehemu gani," alisema Banda anayesifiwa na wadau wa soka kutokana na mafanikio yake kwenye kikosi cha Baroka.
Banda alisema, kiwango cha Ajibu kwa sasa ni kizuri na mahali popote anacheza isipokuwa awe tayari kufanya hivyo licha ya kuwa anatambua maamuzi hayo ni magumu kutokana na misukosuko ambayo wanakutana nayo nje ya nchi kikubwa anachotakiwa kufanya ni maandalizi tu ya kisaikolojia.
"Ni kweli kucheza nje si rahisi kihivyo, lakini kitu kikubwa kinachotakiwa ni utayari tu wa kazi hiyo,"alifafanua.
 
MSIKIE MWENYEWE
Akizungumzia bao lake, Ajibu alisema mbona amefunga sana mabao ya aina hiyo na  bado ataendelea kutupia kama hivyo, iwapo kuna wanaodhani amebahatisha juzi Taifa.
Ajibu alisema bao kama la juzi Jumapili alilowafunga Mbao ni moja tu ya mabao yake makali aliyowahi kufunga kabla ya hiyo juzi.
"Hili sio bao la kwanza kwangu kulifunga kwa namna hii nimewahi kufunga mengi tu huko nyuma wengi wameliona hili kwa kuwa nimefunga kwenye ligi. Unajua wakati ule mpira unakuja akili iliniambia pale nilipo naweza kufunga sasa mpira ulivyokuja ndio ulivyonitengeneza niupigaje ili nifunge basi nikaamua kuruka vile na kufunga," alisema.
Alisema anamshukuru Mungu kwa kuanza msimu vizuri, lakini bado nataka kujituma zaidi ili nifanye mambo makubwa zaidi lengo ni kuisaidia timu yangu na sio lingine.

AMTUMIA SALAMA AMUNIKE
Aidha Ajibu aliseleza kuwa, bado hajakata tamaa kurudi kuitumikia Taifa Stars na kwamba ataendelea kujituma ili kumshawishi kocha wa timu hiyo, Emmanuel Amunike.
"Sijakata tamaa, naamini nitakuja kulitumikia tena taifa nafasi yangu bado ipo muhimu nitaendelea kujituma ili kuonyesha uwezo wangu, bado nina deni kwa taifa langu."