Ajibu ajipange upya, Okwi awatuliza Simba

Muktasari:

Simba tumemwambia Ajibu hatutaweza kumpa Sh 150milioni kama tulivyokubaliana hapo awali anatakiwa kupunguza dau hilo.

Dar es Salaam.Uongozi wa Simba chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Bilionea Mohammed Dewji 'Mo Dewji' wameanza harakati za kufanya usajili kwa wachezaji kutoka katika timu tofauti jambo linalofanywa kwa usiri mkubwa.

Taarifa zinadai kuwa mshambuliaji Ibrahim Ajibu aliachana na dili lake la kujiunga na TP Mazembe baada ya kuwa na ukaribu na Bilionea Mo Dewji anayetaka kumsajili Simba.

Iko hivi, awali kabla Ajibu dili lake la TP Mazembe kumalizika Mo Dewji alikuwa anataka kumpa mchezaji huyo Sh150milioni jambo ambalo baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba kupinga pesa hiyo kuwa ni nyingi na hakuna mchezaji wa ndani mwenye thamani ya pesa hiyo.

Uongozi huo wa Simba umelichukulia suala hilo kama faida dili la TP Mazembe na Ajibu kumalizika na wamemwambia mchezaji huyo akajifikilie upya katika pesa ya usajili ya mwanzo Sh 150milioni hawataweza kumpa na kama watamsajili watampa chini ya hiyo.

"Kimsingi tumemalizana na Ajibu kwa kiasi kikubwa bado zoezi la kusaini tu kwani amekuwa kipenzi cha mmoja wa watu wenye nguvu katika timu yetu lakini ukweli ambao tumemwambia Ajibu hatutaweza kumpa Sh 150milioni kama ambavyo walikuwa wamekubaliana hapo awali anatakiwa ajifikilie tena tutampa chini yake," alidai kiongozi mmoja wa juu wa Simba ambaye hakutaka jina lake lisiwekwe wazi.

Ofisa Mtendaji mkuu wa Simba, Crescentius Magori alisema kuhusu suala la Ajibu wao hawajapewa jina lolote la mchezaji mpya kutoka kocha wao Patrick Aussems.

Magori alisema kuhusu suala la mshambuliaji wao Emmanuel Okwi waliongea naye kuhusiana na mkataba mpya, lakini aliwaomba kwanza wamsubiri atoke katika mashindano ya Matiafa Afrika (Afcon) akiwa na timu yake ya Taifa ya Uganda.

"Alituomba anaomba akacheze katika mashindano hayo ya Mataifa Afrika akiwa mchezaji huru na hatua yoyote timu ya Taifa ya Uganda itakapoishia atakuja kwetu Simba kuzungumza nasi kuhusiana na masuala yake ya mkataba mpya kutokana na hapa ambapo tumeishia wakati huu," alisema.

"Okwi alituomba hivyo kutokana kuwa na ofa nyingi katika Mataifa na timu nyingine mbalimbali kwahiyo ametuomba kwanza akacheze hayo mashindano na kama kuna timu ambayo itamtaka na itakuwa na maslahi mengi kuliko yetu atatufuta na kutuambia kama tunaweza kumpa maslahi hayo lakini chaguo lake la kwanza litakuwa hapa Simba.

"Kuhusu wachezaji ambao wanamaliza mikataba wengi wao wale wa kikosi cha kwanza tumewaongezea mikataba mipya kwahiyo ile presha ya awali tuliokuwa nayo kipindi wamemaliza mikataba imemaalizika kwani walikuwa wanawindwa na timu nyingine," alisema Magori.