Ajibu, Makambo wahamishwa jiji

Muktasari:

Uongozi wa Ruvu umesema upo katika mchakato wa kuzihamisha mechi zao zote za nyumbani dhidi ya Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Dar es Salaam. KAMA mashabiki wa Yanga wanapiga hesabu za kutaka kuona mavitu nyota wao, Ibrahim Ajibu na Heritier Makambo kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, wasahau tu, kwani Ruvu Shooting wamewahamisha jiji.
Ndio, wiki moja na ushei tangu maafande wengine wa JKT Tanzania kuamua kuwahamisha Simba kwenda kucheza mechi yao Mkwakwani Tanga, Ruvu Shooting nao wameamua kuwahamisha Yanga na kuwapelekea mjini Dodoma.
Uongozi wa Ruvu umesema upo katika mchakato wa kuzihamisha mechi zao zote za nyumbani dhidi ya Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na sasa wanapiga hesabu kwa vijana wa Jangwani wanaojiandaa kuvaana nao.
Ruvu walioga mvua ya mabao kwa kufungwa mabao 5-0 toka kwa mnyama wiki mbili zilizopita wakiwa wenyeji kwenye Uwanja wa Taifa, wameshtuka na kutaka mechi yao na Yanga ikapigwe Dodoma jambo linalowafanya kina Ajibu na Makambo pamoja na wenzake wajipange kwelikweli.
Ajibu na Makambo waliozalisha mabao saba kati ya 17 yaliyofungwa na timu hiyo wataanza kuonyesha ladha nje ya jijini wiki chache zijazo watakapoenda kanda ya Ziwa kucheza mechi zao za viporo dhidi yua Mwadui ya Shinyanga na Kagera Sugar ya mjini Bukoba.
Wazee wa Kupapasa hao wamekuwa wakitumia Uwanja wa Taifa jijini Dar kama Uwanja wao wa nyumbani kwa michezo yao na Simba na Yanga kwa vile uwanja wao wa Mabatini kutokidhi  vigezo vinavyotakiwa na Bodi ya Ligi (TPLB).
Ofisa Habari wa Ruvu, Masau Bwire alisema uongozi wao tayari umefanya mawasiliano na Bodi ya Ligi kwa ajili ya ombi hilo ambalo wanaamini litafanyiwa kazi na wataanza na Yanga katika mzunguko wa pili baada ya Simba kuwawahi mchezo wao wa awali..
"Simba tumewachelewa mchezo wetu wa awali sisi ndio tulikuwa wenyeji taarifa zilifika kwa kuchelewa hivyo mashabiki wa Dodoma wakae tayari kuwapokea Yanga wakiwa kama wageni katika mchezo huo," alisema Bwire.
"Tumepokea maombi kutoka sehemu mbalimbali kama Arusha, Mwanza, Tanga ambako tayari tumewahiwa na JKT Tanzania ambao waliamua kuutumia uwanja huo kama uwanja wao wa nyumbani kwa mechi za Simba na Yanga, baada ya kuwahiwa huko tumeona ni bora tuwafurahishe mashabiki wa Dodoma kwa kuwapelekea michezo yetu ya Simba na Yanga," alisema.
"Dodoma ni mahala sahihi kwanza ni makao makuu ya nchi hakuna Ligi Kuu tukaona tuanze kulipa heshima na hadhi jiji la hilo ili liweze kuonekana linauwezo wa kukidhi hata masuala ya michezo kwa kuutumia Uwanja wa Jamhuri ambao unakidhi viwango vinavyohitajika na Bodi ya Ligi kama uwanja wa nyumbani."
Katika hatua nyingine alisema wameanza mchakato wa kukarabati uwanja wao wa Mabatini kuhakikisha unakidhi viwango vinavyotakiwa na Bodi ya Ligi ili waweze kuchezea hapo na kuachana na tabia za kuhangaika viwanja vingine.
"Kilichokuwa kinatuumiza zaidi ni kuwa wenyeji halafu tunaifuata timu ngeni katika uwanja wao wa nyumbani sasa baada ya kuhamishia Dodoma tunapambana na hari zetu kuhakikisha Mabatini inakuwa bora zaidi," alisema.

WASIKIE YANGA
Kwa upande wa Yanga kupitia kwa Mratibu Mkuu wa klabu, Hafidh Saleh alisema hawana chaguo la uwanja ambao utakuwa umepitishwa na Bodi ya Ligi (TPLB) watacheza popote watakapopelekwa kikubwa kinachoangaliwa ni tamko lao.
"Hatuna chaguo Bodi ikiamua lake tunatakiwa kufuata lakini hadi sasa hatuna taarifa yoyote tuliyopewa kuhusiana na mabadiliko hayo tukiipata tutazungumza zaidi, ila sisi kokote freshi," alisema.
Yanga mpaka sasa ipoa nafasi ya tatu ikiwa na alama 26 sawa na Simba, ila wakizidiwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufunga na pia wakiwa na mchezo mmoja pungufu dhidi ya watani zao na miwili kwa vinara Azam yenye pointi 30.