Ajibu, Gadiel, Ndemla wataweza kupindua meza?

SIMBA ina kikosi kipana kinachoongeza ushindani wa namba ndani ya klabu hiyo. Baadhi ya mastaa wanashindwa kutumika kikosi cha kwanza na kuishia kutazama wenzao wakicheza mara kwa mara.

Hata hivyo, pamoja na kukosa nafasi msimu uliopita, uongozi wa timu bado umeendelea kuwa nao msimu huu wa Ligi Kuu Bara baadhi ya mastaa na sasa ni nafasi kwao kujituma na kulishawishi benchi la ufundi kuwaamini.

Mwanaspoti linakuletea mastaa hao ambao ni vipenzi vya mashabiki lakini wamekosa nafasi kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

IBRAHIM AJIBU

Ana kipaji kikubwa lakini kinachowashangaza mashabiki wa soka nchini ni licha ya uwezo wake, kashindwa kutii kiu yao.

Kwenye nafasi yake kwa sasa wapo nyota kama Clatous Chama, Luis Jose Miquissone, Hassan Dilunga na Benard Morrison ambao Kocha mkuu wa timu hiyo, Sven Ludwig Vandenbroeck anaonekana kuwaamini zaidi.

Hawa wamekuwa moto zaidi na kumfanya Ajibu asubiri benchi na kupigania nafasi msimu huu ambao umeanza Jumapili Septemba 6 na kujihakikishia nafasi kama mchezaji muhimu.

SAID NDEMLA

Ni fundi kama tu alivyo Ajibu lakini amekosa nafasi ya kujihakikishia namba na kuonyesha udambidambwi wake ambao mashabiki wanaumisi.

Wamepita makocha kibao Simba lakini wote wamekuwa wakishindwa kumtumia kwa sababu ya kutokujituma.

Ni wajibu kwake sasa kuonyesha uwezo wake kwa benchi la ufundi ili msimu huu aweze kulishawishi na kumpanga na kujihakikishia namba.

GADIEL MICHAEL - SIMBA

Tangu atue akitokea Yanga na kumkuta Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ amepata wakati mgumu sana wa kuanza kikosini kutokana na uwezo wa Tshabalala.

Yanga alikuwa tegemeo lakini ujio wake Simba, itabidi akomae sana ili kulishawishi benchi la ufundi ingawa ni wazi anakipaji kikubwa.

BENO KAKOLANYA

Kipa Beno Kakolanya hajajihakikishia nafasi ndani ya kikosi cha kwanza na mechi nyingi anaonekana kupangwa mpinzani wake Aishi Manula, hivyo huu ni msimu wake wakujituma zaidi ili kubadili upepo wa yeye kuaminiwa kama ilivyo kwa mwenzake.

Beno alitoka Yanga akiwa anaamini na kutegemewa kwenye kikosi cha kwanza, uwezo wake ndio uliwavuta Simba kumpa ajira kwenye kikosi chao. Bado hajachelewa kufanya jambo msimu huu.

MIRAJI ATHUMAN

Huyu ni kama anakuja kwenye mpango wa kocha, majeraha ndio yalikatisha juhudi zake za kupambania nafasi kwenye kikosi cha kwanza, hivyo msimu huu ana kazi ya kujituma kuhakikisha anaaminiwa kuanza mechi.

Ugeni wa msimu ulioisha ndio uliwaaminisha watu, kuona anaanzishwa mechi chache kabla ya kuumia, kuna wakati alikuwa anachukua nafasi ya Meddie Kagere na Francis Kahata.

WADAU WATOA NENO

Mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Zamoyoni Mogella anawataja Ajibu na Ndemla jinsi wanavyomuumiza moyo, kushindwa kuona mamilioni ya pesa yaliopo mguuni kwao, endapo kama watakubali kwenda kwa muda mchache timu watakazoaminiwa.

“Sisi wachezaji wa zamani ni mfano kwao, kwa sababu baada ya kumaliza kipindi chetu hatuna hata mafao tunalipwa kwa kuzipenda hizo klabu, soka sasa ni biashara kubwa sana, hivyo wanapaswa kuangalia fursa kuliko kushabikiwa na mashabiki,” anasema nakuongeza “Ukiachana na hao, alikuwepo na Ibrahim Mohamed yule kijana alikuwa ana kitu mguuni, lakini mwishowe unaona anaondoka kwenye laini ya gemu, ujumbe wangu ni Ajibu na Ndemla wanaongeze mazoezi ni vijana ambao wanaweza wakafika mbali,” anasema.

Naye kocha wa zamani wa timu hiyo, Abdallah Kibadeni anasema hao bado ni vijana wadogo, wasikubali kupoteza thamani yao kwa kukaa benchi kirahisi, wajitume katika mazoezi ili waweze kuwa tishio kwenye kikosi cha kwanza.

“Utayari wa mchezaji unaanzia kwenye mazoezi hiyo mechi inakuwa ni jambo la kumalizia, wakijituma kwa bidii kama vile wanakwenda kucheza fainali ya Afrika halafu wao ndio wachezaji muhimu, naamini msimu huu watabadili upepo,” anasema.