Ajib, Manula waanza mazoezi Simba

Muktasari:

Simba inajiandaa na mchezo wa marudiano Ligi ya Mabingwa dhidi ya UD Songo utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa.

Dar es Salaam. Wachezaji Ibrahim Ajib na Aish Manula wameanza mazoezi baada ya kuwa nje kwa muda kutokana na kupata majeruhi.

Ajib na Manula tangu walivyoitwa katika kikosi cha timu ya Taifa Tanzania, hawakuweza kurejea katika klabu yao ya Simba kutokana na kupata majeraha wakiwa katika majukumu ya Taifa.

Katika mazoezi ya Simba yanayoendelea katika uwanja wa Gymkhana, Manula na Ajib walikuwa sehemu ya mazoezi hayo.

Manula alikuwa akijifua na makipa wenzake, Ally Salum na Beno Kakolanya, huku kocha Mohammed Mwalami akisimamia mazoezi hayo.

Licha ya kutokuwepo muda mrefu, Aish alikuwa akifanya vizuri kila zoezi ambalo alikuwa akipewa na hata alipokuwa anakosea na kuelekezwa alikuwa akifanya vizuri.

Kwa upande wa Ajib yeye alikuwa akifanya mazoezi mengine ambayo yalikuwa yakiendelea na wachezaji wenzake.

Simba inajiandaa na mchezo wa marudiano Ligi ya Mabingwa dhidi ya UD Songo utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa.