INGEKUWA VIPI? : Ajax ingebaki na mastaa hawa tishio hadi sasa bila kuwauza

Muktasari:

Davinson Sanchez  Baada ya kuanza kuzivutia klabu mbalimbali kubwa barani Ulaya hatimaye Tottenham ilimnasa katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2017 kwa dau la Pauni 42 milioni.

AMSTERDAM, UHOLANZI . KATIKA kipindi cha miaka 10 iliyopita, Ajax imeuza mastaa wengi mbalimbali ambao kama mpaka leo wangekuwa bado hapo si ajabu ingekuwa moja kati ya timu bora barani Ulaya.

Jasper Cillessen (Kipa, Barcelona)

Aliichezea Ajax mechi 143 akikipiga kwa miaka mitano hapo baada ya kuunuliwa kutoka klabu ya NEC ya hapo hapo Uholanzi. Hata hivyo, mwaka 2016 aliuzwa kwenda Barcelona kwa dau la Pauni 11.7 milioni. Hata hivyo, amekuwa hana nafasi ya kudumu kikosini.

Davinson Sanchez (Beki, Tottenham)

Beki wa kutegemewa wa sasa wa Tottenham Hotspur. Staa huyu wa kimataifa wa Colombia aliichezea Ajax mechi 45 baada ya kununuliwa na klabu hiyo akitokea Atletico Nacional ya kwao mwaka 2016. Baada ya kuanza kuzivutia klabu mbalimbali kubwa barani Ulaya hatimaye Tottenham ilimnasa katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2017 kwa dau la Pauni 42 milioni.

Toby Alderweireld (Beki, Tottenham)

Beki wa shoka wa kimataifa wa Ubelgiji ambaye amerudisha makali yake kwa sasa. Aliichezea Ajax mechi 186 na kutwaa mataji matatu kiasi cha kuanza kutamaniwa na klabu mbalimbali kubwa barani Ulaya.

Hatimaye aliuzwa kwenda Atletico Madrid katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2013 kwa dau la Pauni 6.3 milioni tu.

Baadaye alikwenda kwa mkopo Southampton kucheza chini ya kocha wake wa sasa, Mauricio Pochettino lakini lilipokuja suala la dili la moja kwa moja alinunuliwa na Spurs.

Jan Vertonghen (Beki, Tottenham)

Inaonekana Tottenham ni moja kati ya timu ambazo zimenufaika na vipaji vya Ajax. Beki huyu mwingine wa shoka wa kimataifa wa Ubelgiji naye ni mmoja kati ya mastaa ambao walitokea Ajax na alicheza mechi nyingi.

Alicheza mechi 220 kabla ya kujiunga na Tottenham katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2012 kwa dau la Pauni 11. 2 milioni.

Kenny Tete (beki kushoto, Lyon)

Beki wa kimataifa wa Uholanzi ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Lyon ya Ufaransa. Alinunuliwa kwa dau la Pauni 2.7 milioni katika dirisha la majira ya joto mwaka 2017 baada ya kuichezea Ajax mechi 55.

Katika msimu wake wa mwisho na Ajax alionekana kukosa nafasi Ajax lakini baada ya kutua Lyon alionyesha makali na kufanikiwa kucheza mechi 31 katika michuano mbalimbali ndani ya msimu wake wa kwanza tu huku Lyon ikishika nafasi ya tatu. Kwa sasa ni chaguo la kwanza katika kikosi cha kwanza cha Uholanzi chini ya Kocha, Ronald Koeman.

Gregory van der Wiel (Beki kulia, Toronto FC)

Mmoja kati ya mastaa ambao waliibukia Ajax. Aliichezea Ajax mechi 187 kabla ya kuuzwa kwenda PSG katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2012 kwa dau la Pauni 5.3 milioni.

Aliichezea PSG mechi 132 katika misimu zaidi ya minne huku akitwaa mataji manne ya Ligi Kuu ya Ufaransa. Van der Wiel vile vile alikisaidia kikosi chake cha sasa cha Toronto FC kucheza fainali ya michuano ya CONCACAF lakini wakapigwa na Guadalajara ya Mexico.

Davy Klaassen (kiungo, Werder Bremen)

Mmoja kati ya watumishi wa muda mrefu walioibukia Ajax ya watoto. Klaasen alitwaa mataji matatu ya Ligi Kuu ya Uholanzi na Ajax na pia alikuwa sehemu ya kikosi cha klabu hiyo ambacho kilifika fainali ya Europa misimu miwili iliyopita. Katika msimu huo alifunga mabao 13 na kupika mengine manane. Katika dirisha kubwa la majira ya joto 2017 aliuzwa kwa dau la Pauni 24 milioni kwenda Everton.

Hata hivyo, mambo hayakwenda vema Everton na alishindwa kuendana na kasi ya Ligi Kuu ya England akianza mechi tatu tu. Everton iliamua kumruhusu aondoke na ikamuuza kwa dau la Pauni 12 milioni tu kwenda Werder Bremen.

Wesley Sneijder (kiungo wa kati, Al-Gharafa)

Mmoja kati ya mastaa wakubwa zaidi kuwahi kuibukia Ajax. Alilitangaza vyema jina la Ajax. Aliichezea Ajax kwa miaka mitano akicheza mechi 180 kabla ya kuuzwa kwenda Real Madrid katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2007 akiuzwa kwa dau la Pauni 24.3 milioni.

Baadaye alikwenda Inter Milan alikotwaa mataji matatu kwa mpigo mwaka 2010 chini ya Kocha Jose Mourinho kisha akaenda Galatasaray na baadaye akatua Nice ya Ufaransa.

Alicheza mechi tano tu katika miezi mitano akaamua kwenda zake Qatar kujiunga na Klabu ya Al-Gharafa. Sneijder ameichezea Timu ya Taifa ya Uholanzi zaidi ya mechi 100 na alikuwa nguzo kubwa wakati ikifika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 ingawaje ilichapwa na Hispania.

Christian Eriksen (kiungo, Tottenham)

Staa mwingine wa Tottenham ambaye ni matunda ya Ajax. Eriksen alitwaa mataji manne ya Ligi Kuu ya Uholanzi na Ajax na kuanza kuwindwa na klabu mbalimbali kubwa barani Ulaya.

Baada ya kuichezea Ajax mechi 162 hatimaye aliuzwa kwenda Tottenham katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2013 kwa dau la Pauni 12.15 milioni.

Dau ambalo alinunuliwa lilikuwa sehemu ya mauzo ya pesa ambazo Tottenham Hotspur Spurs ilivuna kutoka kwa Real Madrid baada ya kumuuza Gareth Bale kwa dau la Pauni 85 milioni ambalo lilikuwa rekodi ya uhamisho wa dunia.

Luis Suarez (mshambuliaji, Barcelona)

Staa mwingine mwenye jina kubwa ambaye ametokea Ajax. Alijiunga na Ajax mwaka 2007 akitokea katika Klabu ya Groningen ya hapohapo Uholanzi ambayo ilikuwa imemchukua kutoka Amerika Kusini.

Akiwa na Ajax alijenga sifa kubwa ya kuziona nyavu mara kwa mara na mwaka 2011 katika dirisha kubwa la majira ya joto aliondoka Ajax baada ya kuichezea mechi 159 na kujiunga na Liverpool akinunuliwa kwa dau la Pauni 23 milioni. Alitisha akiwa Anfield na alifanikiwa kuziba vyema pengo la staa Fernando Torres. Mwaka 2014 aliuzwa kwenda Barcelona ambako amekuwa akitamba mpaka sasa. Tayari ana mataji matatu ya La Liga, manne ya Kombe la Mfalme na katika msimu wake wa kwanza tu alitwaa taji la Ulaya.

Zlatan Ibrahimovic (mshambuliaji, LA Galaxy)

Mkongwe huyo amekuwa na jina kubwa zaidi kutoka Ajax katika kipindi cha miaka 15 iliyopita. Ajax ndio ilimvuta kutoka kwao Sweden alikokuwa anachezea timu ya Malmo mwaka 2001. Aliichezea mechi 110 akitwaa mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uholanzi kabla ya kwenda Juventus katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2004 akiuzwa kwa dau la Pauni 14.4 milioni.

Baadaye alizurura katika klabu mbalimbali kubwa za Ulaya zikiwemo AC Milan, Barcelona, Inter Milan, Paris Saint-Germain na Manchester United. Kwa sasa yupo Marekani akimalizia maisha yake ya soka.

Wacheji wengine waliopita katika miaka ya karibuni- Arkadiusz Milik (Napoli), Riechedly Bazoer (Porto), Ryan Babel (Besiktas), Justin Kluivert (Roma).