Aiyee aziingiza vitani Prisons, KMC, Namungo

Muktasari:

Aiyee ni kati ya wachezaji ambao wanaotarajia kupiga pesa ndefu kwenye usajili wa msimu huu, baada ya kuonyesha kiwango cha hali juu msimu.

Dar es Salaam. Mshambuliaji Salim Aiyee wa Mwadui FC, amegeuka lulu kwa timu za Ligi Kuu Bara, baada ya kumaliza msimu huu akiwa amefunga jumla ya mabao 18, akiachwa kwa mabao matano na Meddie Kagere mfunguaji bora wa TPL.

Aiyee ndiye alikuwa kinara wa mabao kwenye timu yake ya Mwadui FC, huku Kagere akimaliza na 23, jambo hilo limemfanya aonekane huduma yake ya thamani mbele ya timu mbalimbali za ligi kuu Bara.

Tayari Prisons, KMC, Namungo pamoja na timu yake ya Mwadui FC zimeingia katika vita ya kuwania saini ya Aiyee.

Aiyee amekiri kutafutwa na timu hizo, lakini amedai kwamba bado hajakaa chini kukubaliana na timu yoyote akidai anajipa mapumziko baada ya kutoka kwenye kazi ngumu ya msimu.

Mbali na kufunga mabao 18 kwenye ligi, pia mabao yake mawili dhidi ya Geita Gold kwenye mechi ya playoff ambayo yamefanya wabaki ligi kuu.

"Viongozi wa Prisons wamekuwa wakinipigia pigia kutaka nikaitumikie timu yao, lakini pia Mwadui FC wanataka nibaki, bado sijakaa nao mezani kujua nifanye nini.

"Naipa nafasi kubwa Mwadui FC ambao ni timu ilionitangaza kiwango changu mbele ya wadau wa soka nchini, hivyo wakinipa dau tutakalokubaliana nao basi nitabaki la nitaangalia maisha kwingine"anasema.