Aisha asimulia siku ya kwanza na Gadiel

Muktasari:

Mwanaspoti limefanya mahojiano ya kina na mzazi mwenzie na beki huyo, Aisha Haroon, kuhusu maisha yake nje na ndani ya soka ambapo amefunguka namna walivyokutana hadi kuoana.

NI ngumu sana kusikia jina lake likitajwa na mashabiki wa soka nchini, lakini ukitafuta wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Yanga msimu ulioisha, huwezi kuacha kulitaja jina lake. Hapa namzungumzia Gadiel Michael M’baga.

Ni nadra sana kwenye mchezo wa soka kusikia mabeki wa pembeni wakipewa sifa na hii ni kutokana na majukumu yao makubwa uwanjani, kuwatuliza mawinga wa pembeni. Soka limewatenga sana watu hawa lakini hakuna wanachojali wameendelea kupiga kazi.

Leo hii kila kinapotajwa kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ huwezi kumkosa Gadiel Michael, mzaliwa wa Tanga, ambaye kwa sasa alikuwa gumzo katika usajili wa msimu ujao.

Mwanaspoti limefanya mahojiano ya kina na mzazi mwenzie na beki huyo, Aisha Haroon, kuhusu maisha yake nje na ndani ya soka ambapo amefunguka namna walivyokutana hadi kuoana.

ALIVYOJIOPOLEA JIKO

Kila mahusiano yana namna ya kuunganishwa kuna wanaokutana kanisani, kwenye usafiri na wengine wanakutana kazini, basi unaambiwa Gadiel ugonjwa ulimfanya apate mke.

“Mimi na mume wangu tuna miaka miwili sasa tangu tumeanza uhusiano, tulikutana katika mazingira ya kazi mimi ni nesi nilikuwa katika kituo changu cha kazi alikuja kupima na akanikuta mimi hapo ndio ulikuwa mwanzo wa mahusiano yetu.

“Baada ya vipimo alihitaji mawasiliano zaidi hiyo ilikuwa Tanga tulianza kwa mawasiliano ya kawaida hadi sasa nimekuwa mke wake halali kwa ndoa ya kanisani,” anasema.

NI BABA BORA

Pamoja na majukumu makubwa aliyonayo katika soka unaambiwa Gadiel akiwa nyumbani ni baba bora kwa familia yake ambayo ni ya mtoto na mke wake.

“Majukumu ya soka yanaishia uwanjani akifika nyumbani huwa anapenda kukaa pamoja na sisi, lakini kubwa zaidi ni kwa mtoto wake humwambii kitu, muda wote anapenda kuwa naye karibu.

“Shughuli kubwa anayoifanya akiwa nyumbani ni kumwangalia mwanaye yupo katika mazingira gani, muda wote hapendi kuona ni mchafu au anatoa chozi, anajua kumbembeleza hadi akalala,” anasema Aisha.

HUMWAMBII KITU KWENYE MSOSI

Usione kasi yake ya kupanda na kushuka uwanjani ukajua inatokana na mazoezi anayofanya chini ya kocha wake, hapana, unaambiwa anapenda kula huyo. “Mume wangu ukitaka kumkwaza basi onyesha uvivu kwenye kupika, anapenda kula huyo, kwa siku anaweza akala hata mara tano. Yeye muda wote anapenda kuweka kitu mdomoni.

“Anapenda sana wali samaki, ni mtoto wa Tanga hivyo kuhusu wali humwambii kitu anaweza kula mara tano kwa siku na chakula ni aina moja tu,” anasema.

AKIFUNGWA MAUMIVU UWANJANI HADI NYUMBANI

Gadiel katika kitu ambacho kinampa maumivu zaidi basi ni pale anapopata matokeo mabaya uwanjani anachokutana nacho nyumbani ni maumivu pia.

“Mimi sio mpenzi wa mpira hivyo sifuatilii sanaa lakini siku nikisikia timu anayocheza mume wangu imefungwa basi huwa namsubiri kwa hamu akirudi napenda kumtania tu hakuna kingine ninachomfanyia,”

“Huwa anakasirika muda huo tu baadae anarudi katika hari yake ya kawaida japo huwa hawi katika hari ya furaha kama timu yake inaposhinda,” anasema Aisha.