Ai! Defao arudi kwao DR Congo

Muktasari:

Kipindi hicho Defao alikuwa ameachia nyimbo nyingi zilizofanya vizuri sana kutokana na ujumbe mzito wa kuukashifu utawala wa marehemu Laurent.

BAADA ya kuishi nchini Kenya kwa miaka 18 kama mkimbizi, hatimaye mkongwe wa lingala kutoka DR Congo, General Defao karejea kwao.

General Defao alitorokea Nairobi 2001 kipindi ambacho Rais wa zamani Joseph Kabila alipochukua mamlaka kutoka kwa baba’ke Laurent Kabila baada ya kuuawa mwaka huohuo.

Kipindi hicho Defao alikuwa ameachia nyimbo nyingi zilizofanya vizuri sana kutokana na ujumbe mzito wa kuukashifu utawala wa marehemu Laurent.

Hivyo baada ya kuuawa na mlinzi wake, na mwanawe kuchukua usukani, General Defao alihofia maisha yake na kuamua kukimbilia Kenya.

Hata hivyo baada ya Rais mpya Felix Tshisekedi kuchukua utawala kumekuwa na kampeni kubwa katika mitandao ya kijamii kutoka kwa mashabiki wake wakimtaka arudi nyumbani.

Juzi Jumapili, General Defao alifunganya virago vyake na kurudi nyumbani huku akisema alichukua uamuzi huo kufuatia mwaliko wa Rais Tshisekedi.

Ripoti zinaarifu kuwa sasa Defao anapanga misururu ya shoo kuanzia mji mkuu wa Kinsasha kama sehemu ya ukaribisho wake wa kurejea nyumbani kwao.