Aguero azua jambo kwa mwamuzi

Manchester, England. Sergio Aguero ameshutumiwa mitandaoni kwa kitendo chake cha kumshika begani mwamuzi wa pembeni wa kike, Sian Massey-Ellis.

Mshambuliaji huyo wa Manchester City alikuwa akibishana na mwamuzi juu ya mpira wa kurushwa aliowapa Arsenal nja kuishia kumshika begani.

Mwamuzi huyo wa pembeni alionekana kumtoa mkono Aguero na kuendelea na majukumu yake.

Lilionekana kama tukio la kawaida, lakini kanuni iliyowekwa 2016 inaweza kutumika baada ya kuwekwa ili kulinda waamuzi.

Mguso wa aina yoyote kwa mwamuzi wa kati au wa pembeni utaambatana na kadi ya njano kwa atakayefanya hivyo na hata nyekundu, ambayo itategemea amemshikaje.

Lakini Aguero hatapewa adhabu na Chama cha Soka England (FA), ambao walishasema kuwa hakukuwa na mguso wowote wa nia mbaya.

Tangu kutokea kwa tukio hilo, Aguero amekuwa akitolewa maneno na mashabiki wa soka katika mitandao ya kijamii.

Piers Morgan aliandika katika mtandao wa Twitter: “Erm, nini anachofanya Aguero hapa? Na kwanini hakutolewa kwa kadi kwa tukio hili?”

Rosena Allin-Khan naye aliuliza: “Hivi Aguero anadhani yeye ni nani? Hili halikubaliki.”

Wakati huo huo, mwandishi wa soka, Leanne Prescott alisema: “Aguero kugusa shingo ya Sian Massey ni tukio baya.

“Asingeweza kufanya hivyo kama angekuwa ni mwamuzi wa kiume, hili halikubaliki kabisa.”