STRAIKA WA MWANASPOTI : Afrika Mashariki tumejifunza nini kule AFCON?

Wednesday July 10 2019

 

By Boniface Ambani

DUH... Ndio hayo Sasa. Timu zote nne za kanda yetu ya Afrika Mashariki zilitimuliwa katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON).

Uganda ndiyo ilikuwa timu ya mwisho kuondoka katika fainali hizo zinazoendelea kule Misri baada ya kunyukwa bao 1-0 na Senegal.

Ikumbukwe katika mechi za makundi Senegal ilikuwa katika Kundi C pamoja na Tanzania na Kenya. Senegali ilianza na kuitandika Tanzania mabao 2-0 kabla kuichapa Kenya mabao 3-0.

Katika raundi ya 16 bora iliendeleza mziki wake dhidi ya timu zetu za kanda hii baada ya kuichapa Uganda kwa bao 1-0. Inaonekana Senegal ilikuwa inagawa dozi kutonana na vile unavyokuja.

Kwa jumla Senegali imeipa Afrika Mashariki dozi ya mabao masita. Ndipo hapo nami nikapata nafasi ya kuuliza: “Tuliwakosea nini Senegali? Kama kuna uwezekano basi tuombeni msamaha.

Wakati hayo yakitendeka mwenyeji Misri alionyeshwa mlango na Bafana Bafana baada ya kufungwa bao 1-0. Ilikuwa ni kilio. Mohamed Salah hakuamini macho yake wakati Bafana Bafana ilipopiga bao katika dakika za mwisho na kuibuka na ushindi.

Advertisement

Ni aibu kwa mwenyeji kubanduliwa katika mzunguko wa 16 bora. Ukiongeza kwa hayo yaliyo yanaikumba Misri, basi bingwa mtetezi Cameroon akaonyeshwa barabara ya kurudi Yaounde na Nigeria baada ya Alex Iwobi kupiga msumari wa mwisho katika jeneza la mabingwa hao na kufanya mambo yawe 3-2.

Kwa ukweli fainali hizi zimekuwa za kufurahisha. Imekuwa huwezi kutabiri kile ambacho kinaweza kutokea katika michezo hii ya 16 Bora kufuzu kwa robo fainali.

Benin nayo, bila ya kutarajiwa na wengi, ikafanya maajabu yake na kuitimua Morocco mashindanoni.

Kabla watu hawajapumua timu inayoshiriki kwa mara ya kwanza kabisa katika mashindano haya, Madagascar nayo ikaitimua Fimbu ya Fimbu, DR Congo.

Madagascar ikawaambia Wakongo kapigeni densi Kinshasha na mtuache wacheza soka hapa Cairo. Hapa ni soka tu.

Kweli soka halina adabu. Uganda, Cameroon, Morocco, Misri, Congo, Guinea zote zimetolewa kwenye michuano hii.

Hii ni hatari. Timu ambazo watu walikuwa wanazipigia upatu huenda ndizo zingeweza kuchukua ubingwa au kufika mbeli kwenye fainali hizo nazo zimetolewa mapema tu.

Kazi inaonekana bado ni nzito katika michezo iliyobaki baada ya Madagascar kuwashangaza wengi. Pale ilipoitoa DR Congo kwa mikwaju ya penalti. Madagascar inangojea mshindi kati ya Ghana na Tunisia mchezo ambao umechezwa jana usiku.

Hata hivyo, haya mashindano ikiwa yataendelea hivi huenda Algeria inaweza kunyakua taji hili.

Kufuatia matokeo mabaya waliyokutana nayo waandaaji wa michuano hiyo, benchi la ufundi la Misri lililokuwa chini ya Kocha Janivier Aguirre lilivunjwa.

Mbali na Rais wa Shirikisho la Soka la Misri, Hany Abou Rida kulivunja benchi hilo, naye alichukua uamuzi wa kujiuzulu nafasi yake huku akiwataka wajumbe wake nao kufanya hivyo.

Naye kocha maarufu Afrika, Herve Renard ambaye alikuwa akiionoa Morocco kwenye fainali hizo naye amebwaga manyanga.

Renard amekuwa kocha maarufu katika soka la Afrika baada ya kuchukua taji hilo mara mbili akiwa na timu mbili tofauti, kwanza alichukua taji hilo akiwa na Ivory Coast na baadaye akachukua na Zambi.

Kama haitosho katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Kocha wa Uganda Cranes, Sébastien Desabre pia yeye akaondoka. Duh.

Vumbi bado linazidi kutimka AFCON kule Misri. Sisi wa Afrika Mashariki tumebaki wa kuelekeza macho yetu katika runinga kuangalia wenzetu wanavyoendelea.

Je, tumekosea wapi? Tanzania imeondoka bila hata ya pointi moja, Kenya iliondoka na pointi tatu huku Uganda ikifikia hatua ya mtoano ya 16 Bora.

Burundi nayo haikuambulia kitu katika fainali hizo. Je, tumeridhika na kile tulichokivuna?

Kwanza inatupasa tuwe tumejifunza kutokana na makosa tuliyoyafanya, tuangilie timu kama Madagascar inawezaje kufanya vizuri ikiwa ni mara yake ya kwanza tu kushiriki fainali hizo?

Hapa tunapata sababu kubwa ni maandalizi, tuandae mfumo ambao unaweza kutubeba nakuwafanya wachezaji wetu kuweza kupambana na wale wa Afrika Magharibi na Kaskazini.

Haitakuwa busara kama tutafanikiwa kufuzu tena kwa fainali nyingine kisha turudi kama kama tulivyoenda mwaka huu. Hapana lazima tukaze uzi kuanzia sasa kwa kujiuliza, “Tulijifunza nini AFCON”. Siku njema.

Advertisement