Afrika Mashariki tujenge vituo vingi vya soka

Muktasari:

Acha nigeuze kibao katika kanda yetu ya Afrika Mashariki. Ni lini tutaandaa mashindano haya ya Afcon? Ni kizungumkuti. Kisa na maana wengi wa viongozi wetu hawafahamu hasa umuhimu wa kuandaa mashindano kama hayo.

IJUMAA iliyopita ndio Michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) yalifika kikomo kule Misri na Algeria ikitwaa taji hilo kwa mara ya kwanza baada ya kulikosa kwa zaidi ya miaka 29.

Algeria ilitwaa ubingwa huo baada ya kuinyuka Senegal kwa bao 1-0. Furaha ilioje kwa Algiers.

Binafsi niwape hongera kwa kufanikisha ushindi huo kutokana na juhudi zao zilizoanza kuonekana tangu awali.

Wengine lazima tukubali kuwa Algeria walistahili kupata ushindi huo, kwani katika mashindano lazima kuwe na mshindi na mshindwa. Mshindi rasmi ni Algeria ingawaje siye wengine ni washindi katika nyanja nyingine.

Acha nigeuze kibao katika kanda yetu ya Afrika Mashariki. Ni lini tutaandaa mashindano haya ya Afcon? Ni kizungumkuti. Kisa na maana wengi wa viongozi wetu hawafahamu hasa umuhimu wa kuandaa mashindano kama hayo.

Kitu Cha kwanza ni lazima tuanze na kujenga vituo vya soka katika nchi zetu za Kenya, Tanzania, Uganda, Burundi na Rwanda. Ni jambo la muhimu sana kuanza na kujenga sehemu ambazo timu ama klabu zinaweza kufikia pindi zinapofanya ziara katika nchini zetum hapo timu zitapata sehemu ya kufanyia mazoezi.

Vituo hivyo ni lazima viwe vya hali ya juu. Hata kabla kuanza kujenga viwanja vya soka ni lazima vituo hivyo viwepo. Mfano mzuri ni kama Kituo cha pale ‘School of Monetary Studies’ pale Ruaraka, Thika Road jijini Nairobi Kenya. Ni kituo kizuri sana kilicho katika ubora mkubwa unaoweza kuzifanya timu kuweka makazi yake.

Kituo hicho kina kila kitu ambacho unahitaji kukuza vipaji vya vijana wenye umri mdogo. Shida yake ni moja tu ni kukosekana kwa viwanja zaidi ya vitatu. Laiti kama kituo hicho kingekuwa na zaidi ya viwanja vitatu vya mazoezi tungekuwa tunajivunia zaidi.

Kwa hivyo, ni changamoto kwa serekali zetu za Afrika Mashariki, kwa shirikisho la soka Kenya (FKF), Tanzania, (TFF) na Uganda (FUFA), na yale ya Rwanda na Burundi.

Pia, ni changamoto kwa klabu zetu angalau, zinapaswa kuamka sasa nakuonesha ni kweli ziko kwa ajili ya mchezo wa soka. Tunahitaji kutengeneza miundo mbinu ambayo kwa kweli itawapa maofisa wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kuweza kutufikiria na kutupa nafasi ya kuandaa mashindano haya.

Kazi hii inapaswa kuanza kuanzia sasa, sio kila siku mashindano haya yanafanyika Afrika Magharibi au kule Kaskazini tu.

Ikumbukwekuwa mwaka 1996, Kenya ilipaswa kuandaa michuano hii kwa mara ya kwanza lakini ilishindikana baada yake ihakamia Afrika Kusini.

Kenya ilishindwa kwa sababu ya kukosena kwa uwanja wenye hadhi maeneo ya Mombasa. Tena kipindi kile masharti yalikuwa rahisi sana, viwanja viwili tu vya kimataifa.

Tuache tena kufanya mambo ya hovyo, tujipange kuanzia sasa, maana mambo yanavyoenda polepole inafikia hatua wengine tunatamani kuongoza michezo katika Afrika Mashariki.

Shida yetu kubwa hatujui kama michezo ni kitega uchumi cha hali ya juu sana. Hebu fikiria ni pesa kiasi gani wachuuzi pale Misri wametengeneza. Serikali ya Misri, mahoteli, madereva wa teksi, wafanyabiashara wadogo wadogo na wakubwa.

Hebu fikiria Pyramids ziliingiza kiasi gani? Watu wangapi walizuru Misri huu ndani ya mwezi mmoja tu? mashirika ya ndege yaliingiza kiasi gani?

Kitu ambacho hatujui ni kwamba ukitaka kufaulu katika kila jambo lazima uwekeze. Jinyimena umuombe Mungu akufungulie njia. Hatimaye utafika tu.

Kwa hivyo ni mengi ambayo tunapaswa kuyaangalia na kuyawekea mkazo ili Afrika Mashariki iweze kupiga hatua katika soka.

Shida kubwa ya nchi za Kiafrika hususan nchi za kanda yetu ni ufisadi. Ufisadi umekita mizizi hadi unashindwa la kufanya. Kinachotakiwa ni serikali zetu kunyosha mkono wake vizuri, zipalilie vizuri na kuondoa uchafu wote hapo, basi tutakuwa tumebarikiwa.

Mfano mwingine tena kwa Serikali ya Kenya ilisema itajenga zaidi ya viwanja vitano vya soka. Hadi sasa hakuna hata kimoja. Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake William Ruto waliahidi viwanja hivyo. Muda wao unazidi kuyoyoma na hakuna dalili yoyote ya ujenzi wa viwanja umeonekana.

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli ameahidi kujenga uwanja mwingine pale Dodoma na juzi tu amesema uwanja mwingine utajengwa Chato, hivi vitu ndivyo tunavyovitaka katika nchi zetu za Afrika Mashariki. Tupambane ili tuweze kufanikiwa na kuweza kuyaandaa mashindano ya Afcon kwa kukuza talanta na kujenga viwanja. Sio kila siku tunakwenda kukuza uchumi wa watu wengine.