African Lyon watuma salamu kwa Mbao FC

Muktasari:

  • Kipatacho alisema hakuna kingine wanachokitaka katika mchezo huo zaidi ya pointi tatu ambazo angalau zitawatoa mkiani.

VIBONDE African Lyon wametua jijini hapa kuikabili Mbao FC, lakini Kocha Msaidizi, Adam Kipatacho amesema wamekuja Mwanza kwa lengo moja tu la kupata ushindi ambao utawatoa mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Mtanange huo unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba ambapo ni muhimu kwa African Lyon kushinda kwani hadi sasa ina pointi 11 ikiwa nafasi ya 19 kwenye msimamo wa ligi.

Kipatacho alisema hakuna kingine wanachokitaka katika mchezo huo zaidi ya pointi tatu ambazo angalau zitawatoa mkiani.

Alisema kwa sasa hawana mwenendo mzuri hivyo timu yake imeanza kampeni kabambe ya kujinasua kutoka katika eneo la hatari kwenye msimamo wa ligi hiyo hivyo moja ya mechi ambayo ni lazima washinde ni dhidi ya Mbao FC.

“Tumeanza kampeni sasa kila mechi tunataka kupata matokeo mazuri ambayo yatafanya tutoke mkiani kwenye msimamo wa ligi na tunaanza na Mbao FC kuhakikisha tunapata pointi tatu,” alisema Kipatacho.

Alisema wanajua wapinzani wao wametoka kuchezea kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Azam FC na mchezo huo utakuwa mgumu kwao.