Aduda: Huyu Miheso atawanyorosha

Tuesday August 27 2019

 

By Thomas Matiko

Nairobi. OFISA Mtendaji wa Gor Mahia, Omondi Aduda anaamini winga mtalii Clifton Miheso atang’aa ndani ya klabu hiyo licha yake kushindwa kufanya hivyo kwenye timu kadhaa alizochezea nchini na majuu.

Winga huyo wa kushoto anayejulikana kwa kasi yake na chenga za maudhi katalii sana kwenye ligi mbalimbali kabla ya kuamua kurejea nyumbani mwaka huu na kutia saini mkataba wa miaka miwili na Gor.

Baada ya misimu minne tangu 2011 katika Ligi Kuu ya Kenya, Miheso aliondoka Sofapaka 2015 na kujiunga na klabu ya Finland, Vaasan Pallosuera.  Hakukawia sana huko na kuamua kurudi nyumbani na kujiunga na AFC Leopards baada yake kushindwa kung’aa.

Januari 2016 akahamia Golden Arrows inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini ila miezi saba baadaye akavunja mkataba wake na klabu hiyo kwa njia ya utata.

Miheso alidai kulazimishwa kusaini makaratasi ya kuvunja mkataba wake huku akiwa ameshikiwa bunduki. Malalamishi yake yalimgusa Rais wa FIFA, Gianni Infantino na uchunguzi umekuwa ukiendelea.

Baada ya kukaa miezi mitatu bila klabu, Buildcon FC inayoshiriki ligi kuu ya Zambia ikamsajili Machi 2017.

Advertisement

Maisha yake Zambia yalidumu kwa miaka miwili hadi Januari 2019 alipohamia na kujiunga na Olimpico do Montijo inayoshiriki divisheni ya tatu ya Ureno kwa mtakaba wa mwaka mmoja. Hata hivyo baada ya miezi minane kule  alirejea nyumbani na kujiunga na Gor.  Tayari kamfurahisha kocha Steven Pollack ingawaje wadau wengi wamehoji hakuna jipya atakalofanya.

Hata hivyo akitoa mifano, Aduda kawachekea na kuwataka waelewe kuwa Gor ni kiwanda cha mafanikio hivyo hata Miheso, atageuka na kuwa nyota  ndani ya klabu hiyo.

“(Michael) Olunga alipojiunga na Gor wala hakuna aliyekuwa akimfahamu. Kwa wengi alikuwa mchezaji wa kawaida tu aliyezichezea klabu za Thika na Tusker ila misimu michache baadaye kila timu ikawa inakimbizana na sahihi yake. Hivyo ninaweza kukuhakikisha hata huyu Miheso, atanyanyuka tena akiwa ndani ya Gor na mashabiki watampenda,” Aduda kasema.

Advertisement