Adrian mbabe mwingine katika milingoti ya Liverpool

Muktasari:

Yeye ndiye aliyecheza penalti ya staa wa Chelsea, Tammy Abraham na kuipatia ubingwa Liverpool. Ni nani hasa Adrian? Mashabiki wangependa kumfahamu.

LIVERPOOL, ENGLAND. SHUJAA wa Liverpool katika pambano la Super Cup dhidi ya Chelsea alikuwa kipa mpya klabuni hapo, Adrian ambaye mashabiki wengi wa Liverpool bado hawamfahamu vizuri.

Yeye ndiye aliyecheza penalti ya staa wa Chelsea, Tammy Abraham na kuipatia ubingwa Liverpool. Ni nani hasa Adrian? Mashabiki wangependa kumfahamu.

Azaliwa Seville, aanzia ushambuliaji

Jina lake kamili ni Adrián San Miguel del Castillo na alizaliwa katika Jiji la Seville, Hispania Januari 3, 1987. Kwa sasa ana umri wa miaka 32. Alianza kucheza soka katika klabu ya mtaani kwao CD Altair akicheza kama mshambuliaji na winga. Alipofikisha umri wa miaka 10 kipa wao aliondoka na yeye akabadili nafasi kuwa golikipa. Baadaye alisaini katika timu ya vijana ya Real Betis. Alicheza misimu yake miwili ya mwanzo katika timu C na misimu mitano katika kikosi cha wachezaji wa akiba.

Akapelekwa kwa mkopo katika klabu za Alcala mwaka 2008 na Utrera mwaka 2009. Akapelekwa katika kikosi cha kwanza msimu wa 2011–12 akiwa chaguo la tatu huku pia akichezea kikosi B. Novemba akaumia goti ambalo lingemuweka nje kwa miezi mitano na nusu. Alicheza mechi yake ya kwanza ya La Liga Septemba 29, 2012 wakichapwa mabao 0-4 ugenini na Malaga. Hii ilitokana na kipa wao wa kwanza, Casto kutolewa nje kwa kadi nyekundu mapema akalazimika kuingia langoni akichukua nafasi ya mchezaji wa ndani, Salvador Agra. Licha ya kufungwa mabao mengi lakini alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi.

Mechi iliyofuata alianza na kuonyesha kiwango cha juu katika pambano la nyumbani dhidi ya Real Madrid Novemba 24 na kushinda bao 1-0. Kuanzia mechi yake ya kwanza aliyoingia uwanjani, Adrian alicheza mechi 31 zilzofuata klabuni hapo na kuisaidia timu yake kumaliza nafasi ya saba na kufuzu kucheza michuano ya Europa. Mechi 11 kati ya hizo hakuruhusu wavu wake kuguswa.

Atinga West Ham

Akiwa na Betis baada ya kutazamwa na Kocha wa West Ham, Sam Allardyce pamoja na kocha wake wa makipa, Martyn Margetson, Adrián alishawishiwa kujiunga na klabu hiyo. Juni 5, 2013 ilitangazwa kuwa amesaini West Ham kwa mkataba wa miaka mitatu.

Alicheza mechi yake ya kwanza kwa West Ham Agosti 27, 2013 katika pambano la Kombe la Ligi dhidi ya Cheltenham Town ambalo walishinda 2-1. Katika pambano hilo alimchezea madhambi Jermaine McGlashan na kusababisha penalti huku Matt Richards akifunga.

Mechi yake ya kwanza ya ligi ilikuja Desemba 21, 2013 wakichapwa mabao 3-1 na Manchester United nyumbani. Januari 11, 2014 kwa mara ya kwanza alicheza mechi bila ya kuruhusu kufungwa katika pambano dhidi ya Cardiff City waliloshinda 2-0. Mwisho wa msimu alichaguliwa kuwa mchezaji wa pili bora wa msimu nyuma ya Mark Noble. Mpaka kufikia mwishoni mwa msimu wa 2013–14 alikuwa chaguo la kwanza katika lango la West Ham akichukua nafasi ya aliyekuwa kipa wa kwanza Jussi Jaaskelainen.

Bingwa wa penalti kitambo

Katika pambano la raundi ya tatu Kombe la FA dhidi ya Everton Januari 13, 2015 hatua ya matuta, Adrian aliicheza penalti ya kiungo wa Everton, Steven Naismith. Lakini pia akaamua kupiga penalti yake ambayo alifunga ikiwa ni ya ushindi. Kabla ya kupiga penalti hiyo alivua gloves zake akiamini atashinda.

Februari 11, 2015 Adrian alipewa kadi nyekundu katika pambano dhidi ya Southampton baada ya kuudaka mpira nje ya lango kufuatia presha aliyopewa na mshambuliaji wa Southampton, Sadio Mané. Hata hivyo, baadaye aliondolewa adhabu hiyo na FA. Msimu huo alicheza mechi 38 za ligi na nne za FA.

Adrián alipewa tena kadi nyingine nyekundu katika pambano la nyumbani dhidi ya Leicester City walilochapwa 2-1 baada ya kumchezea rafu mbaya Jamie Vardy kufuatia mpira wa kona. Beki wa kulia wa West Ham, Carl Jenkinson ilibidi awe kipa kutokana na West Ham kumaliza mabadiliko ya wachezaji wote.

Oktoba 2015 alisaini mkataba wa miaka miwili klabuni hapo ambao ungemuweka mpaka mwaka 2017. Mwishoni mwa msimu uliopita aliachwa na West Ham huku mechi yake ya mwisho akiwa ameicheza Januari 26 mwaka huu katika pambano la FA dhidi ya AFC Wimbledon ambalo walichapwa 4-2.

Kwa ujumla, katika kipindi cha miaka mitano Adrian ameichezea West Ham mechi 150 na nafasi yake katika kikosi cha kwanza imechukuliwa na kipa wa kimataifa wa Poland, Łukasz Fabiaski.

Liverpool yamnasa bure

Agosti 5, 2019 ilitangazwa Adrian alikuwa amesaini Liverpool bure. Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alikuwa anasaka kipa wa kumsaidia kipa wake, Alisson Becker baada ya kuondoka kwa kipa wa pili, Simon Mignolet aliyerudi kwao kuchezea Brugge.

Ijumaa iliyopita Adrian alicheza mechi yake ya kwanza katika pambano la kwanza la ligi akiingia uwanjani dakika ya 39 kuchukua nafasi ya Alisson ambaye aliumia. Liverpool ilishinda 4-1. Jumatano akawa shujaa katika pambano la Super Cup dhidi ya Chelsea alipocheza penalti ya Tammy Abraham katika hatua ya mikwaju ya penalti baada ya timu hizo kutoka sare ya 2-2.

Aitwa Hispania, ashindwa kucheza

Agosti 26, 2016, Adrian aliitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha wakubwa cha Hispania na kocha wa wakati huo, Julen Lopetegui. Ilikuwa ni kwa ajili ya kujiandaa na mechi dhidi ya Ubelgiji na Liechtenstein lakini hakutumika na hajaichezea Hispania.