Adolf:Tusimlaumu Amunike, wachezaji wetu tatizo

Muktasari:

  • Tanzania sasa watalazimika kushindi dhidi ya Uganda, huku wakiomba Cape Verde ilifunge Lesotho au watoke sare katika mechi ya mwisho ili kufuzu kwa fainali za Afcon2019

Dar es Salaam. Baada ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwaa Lesotho, wadau soka walielekeza lawama kwa kocha mkuu, Emmanuel Amunike, nyota wa zamani wa Stars, Mohamed 'Adolf' Rishard amesema tatizo siyo kocha ni wachezaji.

Stars imefifisha matumaini ya kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) itakayofanyika mwakani nchini Cameroon baada ya kipigo hicho katika mchezo wa marudiano uliochezwa nchini Lesotho Jumapili iliyopita.

Katika mchezo huo, Stars ilihitaji ushindi wowote kujihakikishia kucheza fainali za Afrika, lakini sasa itasubiri hadi Machi 24 mwakani endapo itashinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya Uganda ambayo tayari imefuzu huku ikisikilizia matokeo ya Lesotho na Cape Verde ambapo mojawapo ya timu hizo inanafasi ya kufuzu kwenye kundi L.

Kipigo cha Stars kwenye mchezo wa Jumapili ni gumzo kwa wadau mbalimbali wa soka nchini, huku baadhi yao wakimtupia lawama kocha Amunike kutokana na plani yake ya mechi ya kutumia mabeki wengi kukwama.

Adolf aliyekuwa kwenye kikosi cha Stars kilichoshiriki Afcon kwa mara ya kwanza mwaka 1980, alisema tatizo siyo kocha, wachezaji wetu, tukubali tukatae hawajui mpira au kwa lugha nyingine hawanajitumi.

Alisema katika mchezo wa Jumapili, hakuna mchezaji wa Stars aliyeonyesha nia ya kutaka kufunga kama ambavyo alionekana Mbwana Samatta kwenye mchezo wa marudiano na Cape Verde jijini Dar es Salaam, ingawa Lesotho Samatta hakucheza kutokana na kuwa na kadi.

"Kocha hana tatizo, tatizo ni wachezaji wetu basi, Amunike alipanga timu kutokana na namna alivyowaona wachezaji mazoezini, wanaohoji mbona fulani hakucheza, hawajui alipafomu vipi mazoezini, Watanzania tuache kuingilia majukumu ya kocha," alisema Adolf.

Alisema, jukumu la kuivusha Tanzania ili iweze kufuzu kucheza Afcon ni la wachezaji, kwani wao ndiyo wanaoingia uwanjani, lakini kama hawajitumi, itakuwa ni kazi bure ingawa pia amewasisitiza Watanzania kuwa kitu kimoja kwa kutowatoa mchezoni wachezaji na benchi la ufundi kuelekea kwenye mchezo wa mwisho.

"Kundi bado liko wazi, yoyote kati ya Tanzania, Lesotho au Cape Verde anaweza kufuzu, cha msingi ni kuungana na timu, tuwambie ndiyo wameshindwa kutumia nafasi ya Lesotho, basi ile na Uganda wasiipoteze, kwani mechi hiyo ndiyo itakuwa ngumu kuliko, itafuatiliwa sana, hivyo watulie, wacheze mpira na washinde."