Adi Yussuf aibeba Solihull

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo, alifunga bao hilo katika dakika ya 51 na kuifanya Solihull Moors kujikusanyia alama tatu muhimu ambazo zimeifanya kufikisha pointi 60.

MSHAMBULIAJI wa Kitanzania, Adi Yussuf ameibeba klabu yake ya Solihull Moors ya Ligi Daraja la Nne England kwa kuifungia bao na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ebbsfleet.

Baada ya mchezo huo kumalizika, Adi ambaye ni mzaliwa wa Zanzibar alisema kasi waliyonayo msimu huu, inaweza kuwafanya wafikie malengo yao ya kupanda daraja.

“Niwapongeze wachezaji wenzangu kwa ushirikiano ambao tunaendelea kushirikiana, tunacheza kitimu zaidi, alama tatu kwenye kila mchezo ni kitu muhimu kwetu.

“Tupo nafasi ya pili nyuma ya Leyton Orient iliyotuzidi pointi moja, kikubwa ni utulivu ndani ya timu kwa sababu tunaelekea mwishoni mwa msimu,” alisema Adi.

Mshambuliaji huyo, alifunga bao hilo katika dakika ya 51 na kuifanya Solihull Moors kujikusanyia alama tatu muhimu ambazo zimeifanya kufikisha pointi 60.

MWAMUZI KIBOKO

Maamuzi ya refa, Peter Gibbons, yamezua mjadala baada ya Jumamosi kutoa kadi nne nyekundu katika mchezo kati ya Solihull Moors na wenyeji wao, Ebbsfleet.

Kadi hizo zilitolewa kwenye muda wa ziada ambapo kulitokea mvutano baina ya wachezaji kitu ambacho kilimfanya Gibbons kuanza kumwaga kadi hizo kama njugu.

Walionyeshwa kadi hizo ni Danny Wright na Luke Maxwell wa Solihull Moors huku upande wa Ebbsfleet wakiwa Dean Rance na Bagasan Graham.