Abuu: Njooni tu kwa Benja Afcon yetu

Muktasari:

  • Serengeti Boys imefuzu kucheza fainali za Afrika (AFCON) kwa ya pili. Mara ya kwanza ni mwaka juzi mashindano yalifanyika Gabon na mwaka huu yatafanyika jijini Dar es Salaam.

KIUNGO mshambuliaji wa timu ya vijana chini ya miaka 17, ‘ Serengeti Boys’, Aboubakary Said amesema, wana kila sababu ya kuibuka mabingwa wa fainali za Afrika (AFCON) kwa umri wao zinazotarajiwa kuanza mwezi Aprili na kwenda mbali zaidi.

Aboubakary ambaye ni mwenyeji wa Kisiwani Zanzibar na alichaguliwa kutoka kituo cha kukuzia vipaji vya soka cha JKU.

Alisema, hakuna wanachokiogopa kwa wapinzani wao kwa sababu mpira wanaocheza ni huo huo kikubwa ni ufundi na kufuata maelekezo ya mwalimu wao.

“Tunakila sababu ya kufanya vizuri katika mashindano haya kutokana na maandalizi mazuri tunayofanya. Ninachoweza kusema Watanzania watuunge mkono ili kazi yetu iweze kuwa rahisi,”alisema Aboubakary.

Serengeti Boys imefuzu kucheza fainali za Afrika (AFCON) kwa ya pili. Mara ya kwanza ni mwaka juzi mashindano yalifanyika Gabon na mwaka huu yatafanyika jijini Dar es Salaam.

Katika mashindano hayo yatakayofanyika Aprili 14 hadi 28 nchini, Serengeti Boys imepangwa kundi moja na timu za Uganda, Nigeria na Angola na iwapo itafanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali, itajihakikishia kufuzu Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Brazil.

Serengeti Boys itafungua dimba dhidi ya Nigeria Aprili 14 na baada ya hapo itacheza na timu ya vijana ya Uganda huku mechi ya mwisho ya kufunga dimba ikikutana na Angola.