Abramovich sasa amtaka Pochettino Stamford Bridge

Muktasari:

  • Sari alianza vema Ligi Kuu ya England lakini kadri siku zilivyosonga mbele Chelsea ilianza kupoteza mwelekeo na kwa sasa ni kama vile imejitoa katika mbio za ubingwa ambazo zimebakia kwa Liverpool, Manchester City na Tottenham.

LONDON, ENGLAND.ROMAN Abramovich huwa hataki masikhara na pesa zake. Muda wowote anaamua anachoamua bila ya kusita. Na sasa inadaiwa kwamba kimya kimya ameelekeza nguvu zake katika kumchukua kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino msimu ujao.

Tayari kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri ameanza kukalia kuti kavu baada ya Chelsea kuondoka katika mbio za ubingwa huku akiwa katika hatihati ya kuendelea kubaki Top Four licha ya ushindi wa mabao 5-0 wa Chelsea dhidi ya Huddersfield juzi.

Inasemekana kwamba Sarri amelazimika kumtumia meseji tajiri huyo wa Kirusi kufafanua jinsi fomu ya timu hiyo ilivyopotea baada ya kuchapwa mechi mbili za ugenini mfululizo dhidi ya Arsenal na Bournemouth Jumatano iliyopita.

Kuna uwezekano mkubwa Abramovich akamfukuza Sarri mwishoni mwa msimu kama Chelsea itashindwa kuingia katika Ligi ya Mabingwa msimu ujao wakati huu Arsenal na Manchester United zikiinyemelea kwa kasi nafasi hiyo huku Chelsea wakiwa hawana mwendelezo wa ubora.

Inadaiwa kwamba Chelsea walimfukuzia pia Pochettino katika dirisha kubwa lililopita wakati wakisaka kocha mpya wa kuchukua nafasi ya kocha wao wa zamani, Antonio Conte lakini wakaamua kumchukua Sarri aliyekuwa kocha wa Napoli.

Sari alianza vema Ligi Kuu ya England lakini kadri siku zilivyosonga mbele Chelsea ilianza kupoteza mwelekeo na kwa sasa ni kama vile imejitoa katika mbio za ubingwa ambazo zimebakia kwa Liverpool, Manchester City na Tottenham.

Hata hivyo, Abramovich anatazamiwa kupata upinzani mkali kutoka kwa Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy ambaye anajulikana kwa tabia yake ya kubania watu wake wasiende kwingine kiurahisi. Abramovich anaweza kulazimika kutoa kitita cha pauni 50 milioni kwenda juu kama fidia kwa sababu kocha huyu Muargentina amesaini mkataba mpya wa miaka minne Mei mwaka jana.

Manchester United pia inasemekana inamtaka Pochettino lakini kocha wao wa muda, Ole Gunnar Solskjaer ambaye pia ni staa wao wa zamani ameanza vema maisha yake klabuni hapo na matajiri wa United wanaweza kubadilisha mawazo yao na kumbakisha.

Solskjaer alishinda mechi zake nane za mwanzo na akatoa sare katika pambano lake la tisa dhidi ya Burnley ambapo walikamatwa kwa sare ya 2-2 Old Trafford. Hata hivyo vichapo vyake alivyotoa dhidi ya Arsenal katika michuano ya FA na dhidi ya Tottenham katika Ligi vimeanza kuwafikirisha upya mabosi wa timu hiyo na huenda wakampa kibarua cha kudumu.

Awali Pochettino ilidaiwa kwamba alikuwa anaitaka kazi hiyo ngumu Old Trafford lakini kwa sasa amejikita zaidi katika kuwania ubingwa na na kikosi chake baada ya kutolewa katika michuano ya FA pamoja na kombe la Ligi.

Pochettino ambaye ni kocha wa zamani wa Espanyol na Southampton anapewa sifa kwa kutengeneza kikosi cha ushindani zaidi Spurs licha ya kutopewa pesa za kutosha kununua wachezaji mastaa. Kocha huyo amepitisha madirisha mawili bila ya kununua mchezaji yoyote lakini mpaka sasa Spurs imeachwa pointi nne tu na viongozi wa Ligi Kuu ya England Liverpool.

Kwa misimu miwili iliyopita Spurs wamejikita katika Top Four na hilo limeongeza soko kwa Pochettino ambaye pia amekuwa akihusishwa na Real Madrid ambayo mpaka sasa kama ilivyo kwa Manchester United nayo inamtumia kocha wa muda, Santiago Solari baada ya kufukuzwa kwa Julen Lopetugai mwanzoni mwa msimu huu baada ya timu hiyo kuandamwa na matokeo mabovu.