Abdi Banda mambo ni ‘fire’

Muktasari:

  • Baroka ilikiona cha moto Jumamosi baada ya kutandikwa 2-1 dhidi ya Mamelodi Sundowns wakiwa nyumbani kwenye uwanja wao wa Peter Mokaba uliopo Polokwane.

BEKI wa kati wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Banda mwenye umri wa miaka 24 ameanza mazoezi na kikosi cha kwanza cha Baroka baada ya kupona majeraha yaliyomfanya akosekane kwenye timu hiyo kwa wiki kadhaa.

Banda ambaye msimu huu ameichezea Baroka michezo 13 ya Ligi Kuu Afrika Kusini ambayo ni maarufu kama PSL, anarajiwa kuiongezea nguvu Baroka kwenye safu yao ya ulinzi.

Akizungumzia urejeo wa Banda, Wedson Nyirenda ambaye ni kocha mkuu wa kikosi hicho, alisema anatarajia beki huyo atakuwa msaada kwenye kujinasua kwao wasishuke daraja.

“Sifurahiswi na aina ya matokeo ambayo tumekuwa tukiyapata kwenye michezo ya hivi karibuni, lengo ni kusalia Ligi Kuu. Kuna mambo ambayo nimekuwa nikiyafanyia kazi ili tuweze kufikia lengo.

“Banda ni mchezaji mzuri ambaye naamini kurejea wake kutatusaidia kama timu, nahitaji kuona kila mchezaji akijituma, bado tuna nafasi ya kusogea nafasi za juu,” alisema Nyirenda.

Baroka ilikiona cha moto Jumamosi baada ya kutandikwa 2-1 dhidi ya Mamelodi Sundowns wakiwa nyumbani kwenye uwanja wao wa Peter Mokaba uliopo Polokwane.

Kipigo walichokumbana nacho Baroka ni cha nne kwenye michezo yao mitano iliyopita ambapo mchezo pekee walioshinda ni dhidi ya Kaizer Chiefs kwa bao 1-0, Aprili 06.