Aaah! TFF yaigomea Simba

Muktasari:

  • Manara aliwahi kukaririwa akisema kuwa, Simba endapo wangeshinda dhidi ya Kagera Sugar na Azam FC, basi wangeomba wakabidhiwe kombe wakati wa mechi yao na Sevilla.

HIVI karibuni Msemaji wa Simba, Haji Manara alitoa ushauri kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwamba, kama wataona inafaa basi wakabidhiwe ubingwa wa Ligi Kuu Bara siku watakayocheza na Sevilla inayoshiriki Ligi Kuu Hispania (La Liga).

Simba watakipiga na Sevilla, Mei 22 mwaka huu, kwenye mchezo wa kirafiki iliyoandaliwa na Kampuni ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa ambao, ni wadhamini wa Simba.

Manara ana uhakika kwamba, timu yake itatetea ubingwa wake msimu huu, lakini Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo ameweka wazi kwamba kauli ya Manara ni maoni yake hivyo wadau wa soka akiwemo kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ambaye ameonyesha kukerwa nayo, wanatakiwa kuipuuza kauli hiyo.

Manara aliwahi kukaririwa akisema kuwa, Simba endapo wangeshinda dhidi ya Kagera Sugar na Azam FC, basi wangeomba wakabidhiwe kombe wakati wa mechi yao na Sevilla.

“Tutajaribu kuandika barua kwa TFF ili watukabidhi kombe angalau mechi ambayo tunaona ina hadhi yetu, dhidi ya Sevilla inayoshiriki La Liga,” ilikuwa ni kauli ya Manara kabla ya mechi yao na Kagera Sugar na Azam FC ambapo, walifungwa na Kagera bao 1-0 na kutoka sare tasa na Azam.

Kauli hiyo ilionekana kumchefua zaidi Zahera, ambaye alijibu kiana kuwa: “Simba msimu huu watakabidhiwa ubingwa na TFF, lakini kwa habari ya ushindani sijaona ndio maana Manara anajiamini.”

Kwa upande wa Ndimbo alifafanua kwamba, “Hata Simba wangeandika barua ya kuomba wakabidhiwa taji la ubingwa kwenye mechi dhidi ya Sevilla hata kama itatokea wakiwa mabingwa, hilo halitawezekana kwani mechi hiyo sio ya Ligi Kuu Bara bado ligi haijamalizika, watasubiri hadi mwisho,”.

Beki wa zamani wa Simba, Frank Kasanga ‘Bwalya’ alisema Manara aliongea kama kunogesha gumzo tu kwani, hakuna utaratibu wa kukabidhi taji la ubingwa kwenye mechi za kirafiki tena za kimataifa.

Lakini, akamgeukia Zahera kwa kauli yake kwamba, Simba watapewa ubingwa kuwa sio kauli ya michezo akidai walipokuwa wanaongoza ligi muda mrefu hakulizungumzia.

“Kwanza Simba ni mabingwa hata hao Sevilla watauliza mabingwa wa nchi ni nani, hivyo wanastahili kucheza na timu hiyo ili kupimwa kiwango kama kweli walistahili kuwa mabingwa. Zahera kupambana na wasemaji sio kitu kizuri kabisa kwani, yeye ni kocha, mfano mzuri ni kuwa Simba waliifunga Yanga mechi ya mzunguko wa pili, hivyo aache ulalamishi afanye kazi yake na matokeo yataonekana kwani, soka ni mchezo unaochezwa hadharani,” alisema.