AWCON 2018: Ksh48 milioni zinahitajika maandalizi ya Harambee Starlets

Muktasari:

  • Kenya ambayo iko Kundi B, pamoja na mabingwa watetezi Nigeria, Afrika Kusini na Zambia, itaanza kampeni yake, Novemba 18, mwaka huu dhidi ya Zambia, kabla ya kuwavaa Afrika Kusini (Novemba 21) na baadaye kushuka dimbani dhidi ya wagumu Nigeria, Novemba 24.

Nairobi, Kenya. Jumla ya shilingi 48 milioni zinahitajika kufanikisha maandalizi ya timu ya taifa ya wanawake ya Kenya, Harambee Starlets, inajiandaa na michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AWCON), yanayotarajiwa kutimua vumbi kuanzia Novemba 17 hadi Desemba mosi, mwaka huu, nchini Ghana.
Kwa mujibu wa Rais wa shirikisho la Soka nchini (FKF), Nick Mwendwa ni kwamba, Harambee Starlets, inahitaji fedha hizo kugharamia safari yao kwenda Ghana na Kambi na ambapo FKF imeiomba serikali kuingilia kati kuwasaidia akina dada hao kufanikisha ndoto yao.
Zaidi ya gharama za kuweka kambi, Mwendwa alisema fedha hizo zitatumika kwenye upatikanaji wa vifaa vya michezo, mechi mbili za kirafiki pamoja na gharama za kushiriki michuano hiyo yatakayotimua vumbi siku 26 zijazo.
 “Bajeti nzima ya kugharamia timu kuanzia kwenye maswala ya kambi, vifaa vya michezo na ushiriki wenyewe, ni zaidi ya milioni 48. Tumewasilisha bajeti kwa serikali ili kuona namna ambavyo wanaweza kutusaidia kupata fedha hizo, ili kufanikisha ndoto za Starlets, tunasubiri jibu lao,” alisema Mwendwa.
Aidha, Mwendwa alisema kwa sasa, baada ya kupata uhakika wa kushiriki AWCON 2018, baada ya Equitorial Guinea kufungiwa, FKF iko katika harakati za kutafuta mechi za kirafiki walau mbili, kwa ajili ya kuweka kikosi sawa kabla ya kwenda Ghana ambako watashiriki michuano hii kwa mara ya pili.
Alisema tayari wameshafanya mazungumzo na Uganda ambao wanaonesha nia ya kukubali ombi la kujipima ubavu na Starlets huku pia juhudi kubwa ikifanyika kupata mechi ya kirafiki dhidi ya wenyeji wa makala haya, timu ya taifa ya Ghana.
Kenya ilishiriki michuano yaliyopita ambayo yalifanyika mwaka 2016, nchini Tunisia ambapo Nigeria walitwaa ndoo. Katika michuano hiyo Kenya ilikuwa kundi moja na Nigeria mbapo walipokutana, walipigwa 4-0. Safari hii tena wamewekwa kundi moja.