AWCON 2018: Harambee Starlets, Uso kwa uso na Nigeria tena!

Muktasari:

Kenya inashiriki michuano hii kwa mara ya pili mtawalia, wakipata nafasi baada ya Equitorial Guinea kufungiwa kutokana na kumtumia mamluki kwenye michezo yake. Equitorial Guinea walimtumia Anette Jacky Messomo wa Cameroon katika mchezo wa makundi dhidi ya Kenya.

Nairobi, Kenya. Timu ya Taifa ya wanawake ya Kenya, Harambee Starlets, imejikuta ikiangukia katika mikono ya mabingwa watetezi, Nigeria katika makundi ya Kombe la Mataifa Afrika (AWCON), yanayotarajiwa kuanzia Novemba 17 hadi Desemba mosi mwaka huu.

Kwa mujibu wa ratiba ya michuano iliyotangazwa jana, Harambee Starlets wamepangwa katika Kundi B inayoundwa na mabingwa watetezi Nigeria, Afrika Kusini na Zambia. Wenyeji Ghana wametupwa Kundi A, pamoja na Algeria, Mali na Cameron.

Kuingia katika kundi B, kunamaanisha kuwa, Starlets wana kibarua kizito cha kukabiliana na Nigeria ambalo ni taifa lenye mafanikio zaidi katika michuano hii, baada ya kuibeba mara 10 tangu mwaka 1991. Hii ni mara ya pili kuwekwa kundi moja.

Katika fainali za mwaka 2016, Kenya walikuwa kundi moja na mabingwa hao watetezi ambapo mechi iliyowakutanisha Starlets walioga bakora 4-0. Baada ya hapo Nigeria iliitandika Afrika Kusini 1-0 na kutinga nusu fainali ambako waliitandika Cameroon 1-0, wakabeba Ndoo.