ANARUDI! Mourinho amtaka Ibrahimovic

Muktasari:

Tatizo inaloonekana kwa sasa ni kwamba Ibrahimovic wakala wake ni Mino Raiola, kwa siku za karibuni amekuwa na uhusiano mbaya na Mourinho kufuatia sakata la Paul Pogba na jinsi alivyomwondoa

MANCHESTER, ENGLAND. Vipi kuhusu Zlatan Ibrahimovic. Arudi, asirudi? Mashabiki wa Manchester United watakodoa macho, lakini ndio hivyo dunia inakwenda kasi, mambo mengine hupaswi kuyashangaa.

Kama ulikuwa hufahamu, kinachoelezwa ni kwamba kocha wa Man United, Jose Mourinho anataka kufanya jambo litakalowashtua wengi kwa kumrudisha kwenye kikosi chake, Ibrahimovic kwenye dirisha la Januari. Hivyo ndivyo inavyoripotiwa.

Kwa mujibu wa ESPN, kocha huyo ambaye kiti chake kimekuwa moto kweli kweli huko Old Trafford anamtaka fowadi huyo wa Sweden arudi kwenye kikosi chake baada ya kuonyesha kiwango kikubwa huko Marekani.

Ibrahimovic hakuwa na wakati mzuri katika siku zake za mwishomwisho huko Man United na kubwa lilitokana na majeruhi yaliyokuwa yakimwandama. Lakini, kwa sasa fowadi huyo wa zamani wa PSG na Barcelona, amekuwa mtamu huko Marekani, akifunga mabao 21 katika mechi 25 alizoichezea LA Galaxy inayonolewa na kocha Dominic Kinnear.

Kwa sasa Mourinho anahaha kurekebisha hali ya mambo kwenye kikosi cha Man United baada ya kuanza vibaya kwenye Ligi Kuu England, wakishika nafasi ya nane kwenye msimamo baada ya kukusanya pointi 13, huku wakifunga mara chache kuliko mambo waliyofungwa. Man United imefunga mabao 13 na imefungwa mabao 14.

Lakini, mpango huo umekuwa kama shilingi yenye pande mbili zinazokwenda sawa. Straika, Ibrahimovic naye anaamini Mourinho ndiye kocha sahihi kwenye kikosi cha Man United na atawasaidia wababe hao wa Old Trafford kwenda kubeba taji la Ligi Kuu England.

Katika msimu wake wa kwanza ambao Ibrahimovic alikuwa kwenye kikosi hicho cha Mourinho, alifunga mabao 28 na tangu kuondoka, timu imekuwa na shida kwenye kufunga, huku straika namba moja, Romelu Lukaku akiwa amefunga mabao manne tu kwenye mechi nane alizocheza msimu huu.

Fowadi huyo wa LA Galaxy alisema: "Nadhani ana uwezo mkubwa wa kushinda taji la Ligi Kuu England. Nadhani ndiye mtu sahihi kuwa kocha kwenye klabu hiyo na timu hiyo.

"Lakini, kocha mzuri unaonekana pale timu yako inapokuwa nzuri. Si kwamba ni kitu cha kufanya maajabu kama timu haitakuwa nzuri. Ninachokiona timu itakuwa nzuri, wanaendelea vizuri na watakuwa bora. Huu ni mwaka wake wa tatu hapo na wachezaji wafahamu njia zake za uchezaji na vile anavyotaka wacheze. Hivyo, katika yeye naamini katika neno, ndiyo."

Hata hivyo, katika kuinasa huduma ya Ibrahimovic, Mourinho anapaswa kufanya haraka kwa sababu fowadi huyo yupo kwenye mazungumzo pia na AC Milan ili kurudi kwenye timu hiyo ambayo aliwahi kuitumikia huko Italia.

Shida inayokuja kwa sasa ni kwamba Ibrahimovic wakala wake ni Mino Raiola, ambaye kwa siku za karibuni amekuwa na uhusiano mbaya na Mourinho kufuatia sakata la Paul Pogba na jinsi alivyomwondoa Henrikh Mkhitaryan huko Old Trafford. Wachezaji hao wote hao wakala wao ni Raiola. Kwa Mourinho kufanikisha dili la kumrudisha fowadi huyo kwenye kikosi chake katika dirisha hilo la Januari ili kuja kumpa changamoto Lukaku, anahitaji kumalizana na Raiola kwanza na kusafisha hali ya hewa.

Ripoti za kutoka Old Trafford zinadai kwamba Mourinho kwa sasa yupo kwenye hali nzuri na bosi wake Ed Woodward, ambaye alitibuana naye kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi baada ya kushindwa kumletea wachezaji aliokuwa amependekeza wasajiliwe. Woodward amedaiwa kushindwa kumsajili Ivan Perisic kisa Pauni 3 milioni tu, ambapo Inter Milan walisema kwamba mkataba wa mchezaji huyo utavunjwa kwa Pauni 45 milioni, lakini bosi huyo, ambaye ni makamu mwenyekiti wa Man United alikuwa tayari kulipa Pauni 42 milioni. Matokeo yake, mchezaji wakamkosa na ameendelea kubaki Inter Milan.