MWALIMU KASHASHA: Ambokile anahitaji kujengwa zaidi

Muktasari:

Sambamba na sifa hizo ni kizazi kilichokuwa na moyo wa kujituma, kujitolea na wa kizalendo kwa ajili ya kuzipigania timu zao, ama katika ngazi ya vilabu au hata kwenye timu ya taifa,

Soka ni mchezo unaoishi, na kama ni kweli hakuna ubishi kwamba maisha ya kitu chochote duniani yanatathiminiwa kwa kuangalia kizazi kimoja hadi kingine katika muktadha wa nani alifanya kitu gani kwa wakati wake. Maendeleo ya mchezo huu kwa wapenzi na mashabiki yanajitokeza kwa kuangalia nyakati na vipindi mbali mbali vilivyopita kutokana na matukio yaliyojitokeza na kubaki katika kumbukumbu.
Ni jambo la kawaida hususani kwa wafuatiliaji na wapenzi wa soka kusikia wakisema “ kizazi cha akina fulani……… “ kilikuwa cha hatari mno au kilitisha sana, wakiwa na maana kwamba kuna wakati katika nchi au timu fulani kuliwahi kuwepo na kundi la wachezaji mahiri na mafundi mno ambao walisuuza nyoyo za wapenda soka, na maneno ushindi pamoja na mchezo mzuri yalikuwa ni ya kawaida kwa wapenzi na wafuasi wa timu kutokana na uwepo wa mwendelezo wa kucheza vizuri,kupambana na kushinda katika michezo mingi mbali mbali.
Wapenda soka wa hapa nyumbani licha ya kuzifuatilia timu nyingi za huko Ulaya, bado kwa wale waliokuwepo na kubahatika kuziona timu za hapa nyumbani wanakumbuka jinsi kizazi cha wakati huo katika miaka ya themanini kilivyotisha na kuwapagawisha watu kutokana na uwezo, juhudi na maarifa ya wachezaji. Sambamba na sifa hizo ni kizazi kilichokuwa na moyo wa kujituma, kujitolea na wa kizalendo kwa ajili ya kuzipigania timu zao, ama katika ngazi ya vilabu au hata kwenye timu ya taifa, mathalani kwa kuvitaja vivazi baadhi tunazikumbuka timu za Pan Afrika (1980) ya kina Juma Pondamali, Jella Mtagwa, Gordian Mapango na wengineo au Tukuyu Stars (1987) ya kina Mbwana Makatta, Godwin Aswile, Steven Mussa na wenzao au Yanga (1983) ya kina Hamis Kinye,Yusufu Ismail Bana, Ahamad Amasha na wengineo. Kwa ujumla zama hizi ni za kukumbukwa hadi leo.
Kimsingi inawezekana hatukupata mafanikio makubwa sana lakini bado zipo alama zinazotuonesha kwamba angalao kuna kitu kilikuwa kinafanyika kuashiria maendeleo ya soka kwa mchezaji mmoja mmoja na timu zetu kwa ujumla. Ni wakati huo wachezaji wetu walithubutu kuipeleka bendera ya taifa kwa mara ya kwanza na ya mwisho kwenye fainali za Afcon huko Nigeria mwaka 1980.
Mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika karne hii yanazidi kuamua na kutoa sura na mwelekeo katika mtindo wa maisha ya binadamu, kwa mantiki hiyo sisi pia ni wahanga wa ujio wa mabadiliko makubwa ya kimfumo na mtindo wa kufanya mambo kwa kuwa nchi yetu ni sehamu ya sayari hii ya dunia hivyo hatuwezi kubaki nyuma, tunalazimika kwenda kadri jinsi dunia inavyokwenda ili tuwe sanjali na wenzetu katika mataifa mengine, inawezekana kabisa kuna faida na hasara zake katika kuishi kisasa tofauti na ilivyokuwa wakati huo wa kale.
Ukirejea kwenye zama za kizazi hicho cha dhahabu walikuwepo wachezaji wa aina ya Eliud David Ambokile ambao walifanikiwa kucheza kwa muda mrefu na kwa mafanikio kwa sababu ya namna ambavyo maisha, mifumo na mtindo wa kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji ulivyokuwa tofauti na sasa ambapo sayansi inasimamia na kuendesha mambo.Kimsingi huu ni wakati ambao vipaji vingi vinaibuka lakini havitupatii matokeo na huduma ya kutosha kwa muda mrefu, kila mmoja naweza kuzama katika hoja hii na kuibuka na majibu mengi ya kweli au si kweli.
Wapenda soka wanaofuatilia ligi wanatambua kuwa hadi timu zikiwa zinakamilisha michezo ya mzunguko wa kumi na tatu tunashuhudia kinara wa ufungaji mabao ni mshambuliaji mahiri wa timu ya Mbeya City ya jijini Mbeya mzawa Eliud David Ambokile (21) mzaliwa wa mkoa wa Mbeya wilaya ya Mbeya (V), mchezaji msomi aliyehitimu kidato cha sita katika shule ya sekondari Ivumwe mwaka 2015. Kwa ujumla huyu bado ni kijana mno ambaye anastahili kuangaliwa na kuendelezwa kutokana na kipaji chake ili kiwe ni kwa ajili ya manufaa yake na taifa kwa ujumla.
Ukiangalia historia ya Eliud katika soka bado ni ndogo na hivyo kumfanya aonekane ni mchanga (junior) katika soka la ushindani kwa tafsiri yoyote ile, lakini unaweza kuona ni kwa kiwango gani ameweza kujipambanua katika zama za soka la uwekezaji katika ligi yetu mpaka hapa ligi ilipofikia. Huu ni msimu wake wa pili tangu alipopandishwa kutoka kikosi cha vijana wa Mbeya City na mwalimu wa timu hiyo wakati huo Kinnah Phiri msimu uliopita wa 2017/18 na sasa 2018/19.
Kwa mara ya kwanza wapenzi walio wengi hususani wakazi wa jiji la Dar es Salaam wameanza kumuona kwenye michuano ya Uhai cup iliyojumuisha vijana wa umri chini ya miaka 20 iliyopigwa kwenye dimba la Chamazi Complex ambapo yeye alikuwa ni miongoni mwa vijana waliofanya vizuri na hatimaye kupandishwa kwenye kikosi cha wakubwa. Hii kazi nzuri anayoendelea kuifanya ni matokeo ya uamuzi wa benchi la ufundi na uongozi wa Mbeya City kumuamini lakini pia na kumlea katika misingi bora ya kucheza soka, na yeye kujitambua na kujituma katika kazi hakuna kitu kingine.Hiyo ndiyo imani yangu na wengine kwa mchezaji huyu kuyafanya haya tunayoyaona.Timu ya Mbeya City ikiwa kwenye nafasi ya nane (8) na alama zake kumu na nane (18) kwenye mzunguko wa kumi na tatu, imefunga mabao 15, kwa hesabu za kawaida ina maana yeye peke yake amefunga mabao ya timu yake kwa zaidi ya asilimia hamsini (50%).  Huyu kwa asili ni mshambuliaji lakini ni mfungaji.
 Ligi yetu inao wachezaji wengi wa kutoka nje ama tuwaite wa kulipwa,ambao wengi wanafanya vizuri na baadhi yao ni wachezaji wa kimataifa kwa misingi kwamba wanachezea timu zao za taifa.Kwa misimu miwili au mitatu mfululizo tunawashuhudia wachezaji wa kigeni wakipokezana na wazawa kutwaa zawadi ya mfungaji bora wa ligi , kiatu cha dhahabu (golden boot), ni jambo zuri linalohamasisha ushindani ndani ya vilabu lakini pia kati ya timu na timu, hatua ambayo inatoa nafasi kwa washambuliaji kucheza kwa malengo zaidi wakijua kuwa mwishoni mwa msimu upo uwezekano mchezaji akatengeneza historia yake mpya au kuiendeleza kama ambavyo wamefanikiwa kufanya akina Hamisi Tambwe, Emmanuel Okwi, John Bocco, Simon Msuva na wengineo.
Kwa bahati mbaya soka la nchi yetu bado linakosa mipango mkakati iliyo madhubuti ya kujenga misingi mizuri kwenye vipaji vya wachezaji wengi vijana, ndiyo moja ya sababu kubwa ya wachezaji wetu kushindwa kudumu katika fani lakini pia bado tuna idadi ndogo sana ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi ukilinganisha na idadi kubwa ya vijana wadogo wenye vipaji walioko mtaani wakicheza mpira usiokuwa na miongozo, huu umekuwa ni ugonjwa wetu wa muda mrefu ambao tiba yake haijapatikana.Kutokana na kukosa mwendelezo na mwelekeo sahihi wachezaji wetu wengi wanayaona mafanikio yao makubwa ni kufanikiwa kucheza kwenye vilabu vikongwe vya hapa nyumbani Simba na Yanga.Huu si mtizamo sahihi hata kidogo kwa sababu hata hawa wakongwe licha ya umri mkubwa hawana chochote cha kujivunia katika soka barani Afrika.
Kwa utamaduni wetu uliojengeka kwa miaka mingi kwenye soka la Tanzania mchezaji yeyote akiibuka kama ilivyojitokeza kwa kijana mdogo Eliud akaonesha cheche kwenye ligi licha ya kwamba hata mzunguko wa kwanza haujakamilika, tayari macho, masikio na akili za watu wa mpira zimeanza kuelekezwa kwake ili kujenga mazingira ya kupata huduma yake, na inawezekana haraka iwezekanavyo. Kwa uzoefu tulionao mchezaji akianza kutajwa au kuhusishwa na timu fulani mara nyingi inakuwa hivyo. Tunafahamu hayo ndiyo maisha ya wachezaji nyota popote pale duniani, lakini hapa nyumbani kuna makosa na dosari nyingi katika kutekeleza zoezi hili la kumuhamisha mchezaji.
Ukimtazama Eliud David Ambokile akiwa kiwanjani unabaini kuwa ni kijana mdogo ingawa ana umbile kubwa analostahili kuwa nalo mchezaji  bado anahitaji msaada katika maeneo mbalimbali kama vile ufundi, mbinu, saikolojia ya mchezaji kwa ajili ya kumuimarisha katika haiba ya uchezaji  na mchezo wenyewe ili aweze kuwa mchezaji wa daraja la juu, hii itamsaidia kutimiza ndoto zake. Uwezo alionao ni mzuri lakini anastahili kuongezewa vitu ikiwa ni pamoja na uzoefu wa michezo mikubwa na migumu.
Hongera kwa kamati ya ufundi iliyompendekeza kuwa miongoni mwa nyota walioitwa kwenye kikosi cha wachezaji wa timu ya taifa chini ya umri wa miaka 23.Nafasi hii itazidi kumpa nafasi zaidi ya kujifunza kupitia mashindano makubwa ya kimataifa.Katika hali ya kawaida mchezaji akiitwa katika timu ya umri huu anakuwa amebakiza hatua moja tu kuelekea timu ya taifa ya wakubwa kitu ambacho kinamsaidia sana kujitambua lakini kupata maarifa na mbinu bora zaidi za kucheza akiingia taifa stars kwa vile anakuwa amepata uzoefu, lakini kwa upande mwingine mwalimu wa timu ya taifa anakuwa na mwendelezo wa taarifa zake za kutosha pamoja na rekodi za utendaji wake kiwanjani na nje ya kiwanja tangu akiwa kwenye timu ya vijana.
Kitaaluma  kizazi fulani katika soka ,ni matokeo ya wachezaji kupikwa kwa muda mrefu na wanaopitia katika hatua moja kwenda nyingine (lader procedure ) hali inayowajenga kuwa bora na imara, kwa sasa tunashuhudia vijana wengi wazuri wakipata nafasi kujiunga kwenye vilabu hivi vikubwa ( vikongwe ) tena zama hizi za ujio wa wachezaji wengi wa kigeni wanaishia kukaa benchi hali ambayo inawaumiza kisaikolojia,inawakatisha tamaa na mwisho wake ni viwango kushuka hali inayosababisha kupoteza muda na fursa nyingi mbali mbali kupitia kwenye mchezo wa soka, ni vizuri wawe makini na waombe ushauri kabla ya kuchukua maamuzi ya kukimbilia kwenye hizi timu kongwe kuna madhara yake mengi kwa walio wengi, wafanye tathimini pana ili kujiridhisha juu ya uwepo wao kwenye vilabu hivi vikubwa.