ALANDO: Klabu tano, Sh17 milioni-2

Thursday December 6 2018

 

JUMATANO iliyopita tulianza makala ya nyota wa zamani wa Kagera Sugar aliyepita klabu kadhaa ikiwamo Azam FC, Philip Alando juu ya safari yake kisoka hadi kuibuka kuwa meneja na sasa mratibu kuwa klabu hiyo tajiri nchini.

Makala hii ilipaswa kuendelea jana Jumatano, lakini kwa sababu zilizokuwa nje ilishindikana na tunaimalizia leo Alhamisi kwa kuendelea na mahojiano ya straika huyo aliyepitia klabu tano tofauti na kuvuna Sh 17 milioni kama fedha za usajili wake.

SIMBA, YANGA ZAMTAKA

Kama ilivyo kawaida mchezaji akiwika sana, klabu kongwe za Simba na Yanga huwa hazilazi damu katika kuwania saini yake, hata kwa Alando anakiri alikumbana nalo.

“Hadi Azam inanisafirisha kuja Dar es Salaam, Simba na Yanga zilishaniwinda mno ila nilikuwa na hofu kujiingiza kwao, nilihofia mambo yangu yasingetimia kwani soka halikuwa kipaumbele changu, nilichohitaji kipindi hicho ni elimu kwanza, hivyo nilijua kwa timu hizo nisingetimiza ndogo yangu ya kusoma.

“Hata nilipofika Dar es Salaam kabla ya kumalizana na Azam, waliposikia walinifuata ili nikubali kusajili kwao ila nilizogomea. Sikuhitaji mpira kuliko elimu, walijaribu hata kunifuata hotelini kunishawishi ila haikuwezekana, niligoma nikasaini Azam ambayo ilinitoa huko Kanda ya Ziwa,” anafichua.

ALIVYOTUA AZAM

“Marehemu Silvester Marsh na Dos Santos ndiyo waliochangia kutua Azam, wao waliniona nikiwa Kagera Sugar, hivyo waliwaambia Azam, nadhani baada ya mazungumzo yao na Azam kusema wanataka mshambuliaji.

“Tulikuja kucheza Dar es Salaam na Manyema na baadaye nilipigiwa simu na kutumiwa tiketi ya ndege, aliyenipokea uwanjani na kunipeleka hotelini ni Nassoro Idrissa ‘Father’ nilisaini mkataba.

“Ukweli sikufurahia kuja kucheza Azam ila nilifurahia kupata nafasi ya kuishi Dar es Salaam ili nitimize ndoto yangu ya kusoma maana hapa kuna vyuo vingi. Moja ya mambo ambayo niliwaweka wazi Azam kuwa nahitaji elimu ya chuo, hivyo kwenye mkataba nisibanwe ili nipate muda wa kwenda chuoni, walikubaliana na mimi.

“Azam ni waungwana ndiyo maana walikubali pamoja na kuwa nipo kwenye ajira yao na sikuitumikia ajira hiyo kwa muda mrefu kwani ndiyo kwanza nilikuwa mgeni kwenye timu,” anasema Alando

CHANGAMOTO YA NAMBA

Alipotua Azam alikutana na washambuliaji kama Nsa Job, Kally Ongala, Ouma kutoka Kenya, Peter Ssenyonjo na Yahya Tumbo wakati huo John Bocco alikuwa anacheza namba nane na saba, hivyo hakuwa na madhara kwake.

“Unajua nikiwa fiti nilikuwa sikai benchi hata siku moja maana nilicheza kwa kiwango bora, ila baadaye nilipata majeraha ambayo yalinisababisha niwe naanzia benchi ingawa roho haiukuniuma kwani lengo langu halikuwa kucheza mpira, bali ni kusoma, hivyo niliona kawaida tu, hao walinipa changamoto ila haikuwa kubwa.

“Bocco ni mchezaji asiyekata tamaa, anajituma, anajitambua, anapenda kazi yake na anaheshimu mpira, ndiyo maana anafanikiwa katika hilo, sikucheza nafasi moja na Bocco japo baadaye alianza kutumika kama mshambuliaji, hiyo yote ni kwa vile ana juhudi binafsi.”

KUSTAAFU

Alando anacheza soka la ushindano kwa miaka mitano pekee akaamua kustaafu, yeye anaelezea kwanini alistaafu soka angali bado alikuwa na uwezo wa kucheza.

“Kama nilivyosema sikuwa na malengo na mpira, watu ndiyo walikuwa wanaona nina kipaji cha kucheza, 2010 niliacha rasmi, baadaye ya kustaafu uongozi wa Azam ulinipa nafasi ya umeneja timu ya vijana na baadaye walinipandisha hadi timu kubwa kuwa meneja mkuu, hizo zote ni faida ambazo nimezipata ndani ya Azam na sidhani kama ningezipata kwenye timu nyingine.”

Alando anamtaja Juma Kaseja aliyewahi kuzidakika Simba, Yanga, Moro United, Mbeya City, Kagera Sugar na sasa KMC kama mmoja ya makipa hodari nchini aliyewahi kumtungua mara nyingi.

“Nimecheza na Kaseja tangu nikiwa Umiseta tulikutana mara nyingi akiwa na timu yake mimi nikiichezea Kanda ya Ziwa, nikiwa Pallsons ya Arusha, AFC, Toto, Kagera, Azam wakati huo yeye anaichezea Yanga. Ingawa sina rekodi lakini nimeshamfunga Kaseja magoli mengi kuliko mchezaji mwingine yeyote.

“Yeye anafahamu jinsi gani nimemfunga tangu tunacheza huko chini, namfahamu vizuri sana,” alisema.

KIKOSI CHAKE

Hadi sasa wachezaji ambao amecheza nao baadhi yao bado wanaendelea kucheza mpira ambao ni Kaseja, George Kavila, Paul Ngway, Paul Nonga, Shaaban Nditi, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Dickson Daud, Mau Bofu, Aggrey Morris, Jamal Mnyate, David Mwantika, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Himid Mao na Bocco.

“Wengine nimecheza nao timu moja kwenye baadhi ya timu nilizopita, ila wengine tulikuwa tunakutana katika mechi za ligi, wengi wao viwango vyao bado vipo juu kwani walikuwa wanapenda soka tangu mwanzo, mi sikuupenda ndiyo maana safari yangu iliishia njiani.”

Kuhusu ufungaji bora, anasema amewahi kuwa mfungaji bora mara mbili akiwa na Toto African na AFC.

“Nikiwa AFC nilimaliza na mabao 11, japo kwenye ligi nzima tulifungana watatu mimi na wengine wawili kutoka Simba na Mtibwa Sugar, zawadi ilienda kwa mmoja wao sikumbuki wa timu ipi.

“Nikiwa Toto nilimaliza na mabao tisa, ingawa hapa sitasahau kwani mechi ya mwisho nikiwa na mabao saba, Michael Katende alikuwa na mabao tisa. Mechi ya mwisho tulicheza na Ashanti United katika mechi hiyo nilifunga mabao mawili na kufikisha tisa na kabla mechi haijaisha nilikosa bao baada ya mwenzangu kupiga mpira niliotaka kufunga na kutoka nje baadaye Katende akafanikiwa kuifungia mabao mawili timu yake na kunipita.

“Nilitokwa machozi kwa uchungu kwani nilijua ningechukua kiatu cha dhahabu ila kilienda kwa Katende, hivyo ndivyo mpira ulivyo unaweza kupanga jambo lakini likaharibika kabla ya kufikia malengo.”

MAKOCHA BORA

Amepita kwenye mikono ya makocha 11 katika timu tofauti alizocheza ambao ni Marehemu Syllesaid Mziray, Juma Pondamali, Abdallah Kibadeni (wote Pallsons), James Bukumbi, Charles Kilinda, Marehemu Marsh, Dos Santos, Idd Cheche, Itamar, Stewart Hall na Madukwa aliyemfundisha timu ya Umiseta ya Kanda ya Ziwa.

“Sikuwahi kujuta kuwa chini ya makocha hao, walinifundisha, niliwaelewa lakini zaidi namshukuru Kocha Madukwa kwani bila yeye sidhani hata ningefika Azam.”

Alando anaweka wazi pamoja na timu kubwa hapa nchini ndizo zinazoongoza kusajili wachezaji wa kigeni, lakini anasema kwa asilimia kubwa nyota hao wamefeli.

“Wachezaji wengi wa kigeni wanaidharau ligi ya hapa ndio maana wengi wanafeli kufikia malengo na kuachwa kabla ya kusajiliwa wengine, ligi ya hapa inahitaji mchezaji anayeiheshimu na kujituma.”

“Wachezaji wanapaswa kujitambua hasa wanaouchukulia mpira kama ajira yao tofauti na wale wenye malengo kama niliyokuwa nayo awali kuwa mpira haitakuwa kazi yangu ya moja kwa moja kwenye maisha.”

USAJILI UKOJE

“Zamani mchezaji alisajiliwa hata timu tatu tofauti, maana hakukuwa na mfumo mzuri wa usajili ingawa baadaye walikuwa wanakubaliana ama kutoa adhabu ama wanatumia busara kumaliza matatizo ya usajili, hakukuwa na pesa kama ilivyo sasa.

“Hivi sasa wachezaji wanapata pesa nzuri, haki zao wanapewa na mfumo wa usajili pia ni mzuri kwani hakuna udanganyifu wowote unaojitokeza na ikitokea basi adhabu yake ni kibwa jambo ambalo limefanya kuwepo na nidhamu ya usajili kwa kufuata kanuni na sheria zote.”

Advertisement