AJIBU : Jinsi tulivyojichimbia kaburi Serengeti Boys

Muktasari:

  • Ilichapwa mabao 5-4 dhidi ya Nigeria kwenye mechi ya ufunguzi, ikalala 3-0 dhidi ya Uganda katika mechi yao ya pili kabla ya jeneza lake kupigiliwa msumari wa mwisho kwa kichapo cha 4-2 dhidi ya Angola juzi Jumamosi.

Dar es Salaam.SAFARI ya Timu ya Taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana chini ya Umri wa miaka 17 (AFCON U17) imefikia kikomo juzi Jumamosi baada ya kuchapwa mabao 4-2 dhidi ya Angola kwenye mchezo wa mwisho wa Kundi A la mashindano hayo.

Kipigo hicho kimeifanya Serengeti Boys ambayo iliingia kwenye mashindano hayo kama timu mwenyeji imalize ikiwa haina pointi hata moja, ikifunga mabao sita na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 12 ikiwa ni wastani wa mabao manne (4) kwenye kila mchezo.

Ilichapwa mabao 5-4 dhidi ya Nigeria kwenye mechi ya ufunguzi, ikalala 3-0 dhidi ya Uganda katika mechi yao ya pili kabla ya jeneza lake kupigiliwa msumari wa mwisho kwa kichapo cha 4-2 dhidi ya Angola juzi Jumamosi.

Tumepiga hatua kurudi nyuma

Mwaka 2017, Serengeti Boys ilipata nafasi ya kushiriki Fainali za AFCON U17 zilizofanyika Gabon ambako ilimaliza ikiwa nafasi ya tatu kwenye Kundi B lililokuwa pia na timu za Mali, Niger na Angola ikiwa na pointi nne.

Ilimaliza ikiwa na pointi sawa na Niger iliyomaliza kwenye nafasi ya pili, lakini wapinzani wao hao walifuzu Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo zilizofanyika India kutokana na kigezo cha matokeo mazuri kwenye mechi baina yao ambayo Niger iliichapa Serengeti Boys kwa bao 1-0.

Fainali zile zilipaswa kuwa kama funzo kwetu kwa ajili ya kujipanga na kufanya maandalizi mazuri ili tufanye vizuri katika mashindano yaliyofuata ambayo ni haya yanayofanyika nchini mwaka huu, lakini mwisho wa siku tumeondoka mapema bila pointi huku tukiwa tumebebeshwa kapu la magoli.

Tulipiga hatua moja mbele wakati ule, na sasa, badala ya kuendelea, tukaamua kupiga hatua 10 nyuma.

Tatizo liko wapi?

Kuna sababu nyingi zinazoonekana kuigharimu Serengeti Boys hadi ikashindwa kufanya vizuri kwenye fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17.

Miongoni mwa sababu hizo ni kutotumia vyema muda na mashindano ya maandalizi katika kuijenga timu. Wakati mataifa mengine yakitumia mechi za kuwania kufuzu na zile za kirafiki kama sehemu ya kufanyia tathmini vikosi vyao, sisi tuligeuza mashindano hayo kama sehemu ya kutafuta mafankio na sifa pasipo kutazama nini kinakuja mbele.

Hilo limezisaidia baadhi ya nchi kuingia kwenye mashindano zikiwa na vikosi imara na vyenye ushindani huku sisi tukiamini tuna timu nzuri kisa ilikuwa inafanya vizuri jambo ambalo limetugharimu.

Lakini sababu nyingine ni ufanisi wa kiwango cha kawaida wa benchi la ufundi. Benchi hilo la ufundi lilikosa mbinu za kung’amua ubora wa timu pinzani na udhaifu wao kwa haraka na kuufanyia kazi.

Kitendo cha Serengeti Boys kupoteza mechi mbili dhidi ya Nigeria na Angola huku ikiwa imetangulia kuongoza (iliongoza 4-3 dhidi ya Nigeria na ikaongoza 2-1 dhidi ya Angola kabla ya kupoteza zote), ni ishara tosha ya namna benchi lake la ufundi lilivyoshindwa kutafuta mbinu bora ya kulinda matokeo iliyoyapata.

Lakini pia kuna sababu nyingine ya kilichotukwamisha ni mfumo wa kupata wachezaji wa kuchezea Serengeti Boys pamoja na changamoto kadhaa za kiutawala.

Nini kifanyike?

Hakuna namna unayoweza kuwa na timu bora ya taifa kama hauna wachezaji wazuri na wanaoweza kumudu ushindani kutoka kwenye klabu mbalimbali.

Nchi zote ambazo zinafanya vizuri kwenye soka la vijana ni ama zina vituo bora vya kulea na kutunza watoto wenye vipaji vya soka au wana ligi imara za vijana.

Kwa nchi yetu dalili za kupata vituo vya daraja vya juu vya kutunza vijana wenye vipaji kwa kipindi hiki hazipo hivyo suluhisho pekee ni kuwa na ligi ya vijana ambayo itashirikisha vikosi vya vijana chini ya umri wa miaka 17 vya klabu za Ligi Kuu na vinginevyo.

Lakini pia tuimarishe viwango na ufanisi wa makocha wetu wazawa kwani wao ndiyo wanaibua watoto kutokea ngazi za chini.

CECAFA ijitathmini

Baada ya Serengeti Boys kuanza vibaya fainali za AFCON U17, vijana wa Uganda ‘Uganda Cubs’ angalau walianza kuonyesha matumaini kuwa wanaweza kuwa wakombozi wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Hata hivyo, sare ya bao 1-1 dhidi ya Nigeria imeitupa nje timu hiyo na kufanya timu zote za ukanda huu kuaga mapema mashindano hayo.

Hii inatoa picha kuwa mashindano ya kuwania kufuzu fainali hizo yaliyoshirikisha nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati yalikuwa hayana ushindani na dhaifu kiasi cha kuleta timu zilizogeuka kuwa wasindikizaji.

Wakati umefika sasa kwa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kujitazama upya na kuandaa mpango madhubuti ambao utauafanya ukanda huu kuwa tishio kwenye mashindano ya vijana.