AFYA GOGORO : Mastaa hawa trip shamba, trip gereji

Muktasari:

Lakini, wakati Barcelona ikihaha kuziba nafasi yake, Dembele anaingia kwenye orodha ya wachezaji wenye miili ya glasi ambao maisha yao ya soka yametawaliwa majeraha, yaani wako kama magari ya mkaa trip shamba, trip gereji.

BARCELONA, HISPANIA. BARCELONA imetuma ripoti ya daktari inayoelezea ukubwa wa tatizo la Ousmane Dembele kwenda kwa uongozi wa Bodi ya La Liga. Ili iruhusiwe kusajili mchezaji mwingine wa kuziba nafasi yake.

Inaelezwa Dembele, 22, amerudi Barcelona karibuni akitokea Finland, ambako alifanyiwa upasuaji na Dokta Lasse Lempainen ili kutibu jeraha la nyama za paja alilolipata wakati akiwa mazoezini Februari 3, mwaka huu.

Ripoti hiyo imeelezea aina ya jeraha alilolipata, aina ya upasuaji aliofanyiwa na muda ambao anatarajiwa kukaa nje – ambao ni miezi sita, utaratibu unaeleza La Liga itatakiwa kufanya uamuzi saa 72 baada ya kupokea ripoti hiyo.

Kikubwa ambacho Barcelona inataka ni La Liga kuipa ruhusu ya kusajili mchezaji wa kuziba pengo la Dembele ambaye atakaa nje kwa muda mrefu sana kutokana na ukubwa wa jeraha lake.

Kanuni zinaeleza wazi kuwa timu inaruhusiwa kusajili mchezaji wa kuziba nafasi ya majeruhi ikiwa atakaa nje kwa zaidi ya miezi minne, lakini mchezaji hatakiwi kutoka nje ya nchi husika.

Lakini, wakati Barcelona ikihaha kuziba nafasi yake, Dembele anaingia kwenye orodha ya wachezaji wenye miili ya glasi ambao maisha yao ya soka yametawaliwa majeraha, yaani wako kama magari ya mkaa trip shamba, trip gereji.

Ousmane Dembele

Barcelona

Mechi 63

Hii si mara ya kwanza kwa Dembele kukaa nje muda mrefu kutokana na majeraha, mwaka 2017 alikaa nje kwa miezi minne baada ya kufanyiwa upasuaji kama huu wa nyama za paja na Dokta Lempainen, lakini inaonekana safari hii tatizo ni kubwa zaidi kutokana na kutakiwa kukaa nje kwa miezi sita.

Katika maisha yake ya soka hadi sasa tayari Dembele amewahi kukosa jumla ya mechi 63 kutokana na majeraha na idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka zaidi safari hii ambayo anatarajiwa kukaa nje kwa muda wa miezi sita.

Kingsley Coman

Bayern Munich

Mechi 70

Coman amekuwa akisumbuliwa na matatizo mbalimbali kuanzia goti, kigimbi, misuli, lakini tatizo la enka ndiyo huwa linamtesa zaidi kuna wakati aliwahi kukosa mechi 15, lakini pia hilo tatizo limewahi kumkosesha mechi 16.

Hii inamfanya kutumia muda mwingi zaidi hospitali kuliko uwanjani, japokuwa anapokuwa uwanjani huwa ni moto wa kuotea mbali kiasi cha kuwasahaulisha mabosi wake juu ya majeraha yake ya mara kwa mara.

Eric Bailly

Manchester United

Mechi 72

Wakati Man United ikiendelea kuteseka kutokana na beki yake kuruhusu mabao rahisi, Eric Bailly ameendelea kukosekana kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.

Majeraha ya enka na goti kwa nyakati tofauti ndiyo yamewahi kumuweka nje Bailly kwa muda mrefu zaidi, kati ya Julai 25, 2019 tu Desemba 26, 2019 amekosa mechi 28 kutokana na kufanyiwa upasuaji wa goti, wakati kati ya Novemba 2017- Februari 2018 alikosa mechi 21 kutoka na majeraha ya enka.

Neymar

Paris Saint Germain

Mechi 87

Kuna wakati analaumiwa kuwa huwa anajivunja ili akose baadhi ya mechi na kupata wasaa wa kusheherekea sikukuu yake ya kuzaliwa na ile ya dada yake. Huyu naye amekuwa akiteswa na majeraha ya aina nyingi kuanzi enka hadi majeraha ya kanyagio, na haya ndiyo yanamuewekuwa yakimuweka nje mara kwa mara kuna wakati alikosa mechi 18 kutokana na jeraha la kanyagio.

Gareth Bale

Real Madrid

Mechi 109

Moja ya sababu zinazomfanya achukiwe sana na mashabiki wa Real Madrid ni majeraha ya mara kwa mara na ndiyo maana Kocha Zinedine Zidane amekuwa akijaribu kumuuza bila mafanikio. Jeraha ambalo limewahi kumkosesha mechi nyingi zaidi ni la enka ambalo lilimsababisha akose mechi 17 kati ya Novemba 2016 hadi Februari 2017, lakini kwa ujumla Gareth Bale amekuwa mtu wa kucheza mechi tatu na kukaa nje sita.

Andy Carroll

Newcastle United

Mechi 184

Straika huyu wa zamani wa Liverpool ana mwili mkubwa sana, lakini utadhani kaumbwa na glasi maana ukimgusa tu shida, majeraha yake kuanzia ya nyonga, kuvunjika, huku majeraha ya kuvunjika na goti yakichangia kwa kiasi kikubwa kukaa nje muda mrefu, kuna wakati akiwa West Ham upasuaji wa goti ulimuweka nje katika mechi 25, kuvunjika sehemu ya kukanyagia kulimuweka nje katika mechi 23.

Jack Wilshere

West Ham

Mechi 204

Kama kuna kipaji kikubwa sana cha soka kimepotezwa na majeraha basi ni cha Jack Wilshere. Tangu Oktoba 23, 2019 hadi leo yuko nje kutokana na majeraha ya nyonga akikosa mechi 18, lakini Wilshere kwa nyakati tofauti amekuwa akiteswa na majeraha ya enka, goti, kuchanika kwa nyama, kuvunjika na kigimbi ambacho kimewahi kumkosesha jumla ya mechi 47 akiwa Arsenal.