AFYA: Kucheza soka na maumivu ni hatari sana

Muktasari:

Aliendelea kumweleza mwenzake amekuwa akipatwa na maumivu hayo kwa muda mrefu lakini anakomaa hivyo hivyo.

KWA wapenzi wa soka hapa Bongo masikio yapo katika mashindano ya soka Kombe la Mapinduzi yanayoendelea visiwani Zanzibar kwenye Uwanja wa Amani.

Katika pitapita zangu, masikio yangu yalinasa kihabari kilichokuwa kinasimuliwa na mmoja wa mchezaji wa timu (jina kapuni) wa timu iliyoshiriki kuwa alicheza akiwa na maumivu.

Aliendelea kumweleza mwenzake amekuwa akipatwa na maumivu hayo kwa muda mrefu lakini anakomaa hivyo hivyo.

Katika soka mambo kama yapo, mchezaji kwa hiyari yake au kwa kulazimishwa kucheza huwa ni kawaida kucheza ama kuchezeshwa huku akiwa na maumivu ya majeraha ya misuli.

Lakini wengi hawajui kucheza soka huku ukiwa na maumivu ya jeraha ni sawa na kuzima moto kwa petroli, matokeo yake ni huwa moto utaongezeka na kuwa mkubwa zaidi.

Kwa mchezaji kujiongezea jeraha juu ya jeraha huwa inakula kwake kwani jeraha huongezeka ukubwa jambo linaloweza kumfanya kuwa na majeraha sugu.

Hali hii ndiyo inayosababisha wanasoka hasa wale wategemewa katika timu kuwa katika hatari ya kupata majeraha ya mara kwa mara kwani kabla ya kupona vizuri hujijeruhi tena.

Wanamichezo wengi hupatwa na majeraha mbalimbali wakati wa kucheza ikiwamo kuchanika misuli, michubuko, kuvilia damu, kuteguka viungo na kuvunjika mifupa ya mwili.

Ni sahihi kutumia dawa hizo unapokuwa na maumivu kiasi?

Tatizo linakuja wanapotumia holela wa dawa za maumivu ambazo zipo madukani, dawa hizi huwaondolea maumivu kwa muda tu lakini si kuponya jeraha au kupunguza ukubwa wa jeraha.

Leo nitawapa ufahamu wa mambo mawili muhimu kwa wachezaji yaani madhara ya kucheza na maumivu na utumiaji wa dawa za maumivu kiholela.

Kwa nini unatakiwa kuepuka kucheza na maumivu?

Maumivu kwa mwanamichezo aliye majeruhi ni ishara kuwa jeraha bado halijapona vizuri.

Maumivu yanaweza kuwa ya kawaida, ya kati na makali. Yanaweza kuwa ni majeraha ya mfupa, misuli, mishipa ya fahamu na tishu nyingine za mwilini.

Panapotokea jeraha mwili hujibu mapigo kwa kutuma askari mwili kwa ajili ya kukarabati neneo hilo. Mlipuko wa kinga ya mwili ndio chanzo cha mtu kuhisi maumivu, kufa ganzi, kuvimba, kupata joto na kubadilika rangi ya ngozi. Hali hii ndio kitabibu huitwa inflammation.

Wanamichezo ambao wako nje ya uwanja kwa kuwa majeruhi hudhani kuwa maumivu yanapopungua tu wamepona na wako fiti kuanza kucheza. Pasipo kufahamu kuwa jeraha bado halijapona vizuri.

Mara yingine misuli ya mwili ya mwanamichezo inapotumika sana huambatana na vimichubuko vya ndani kwa ndani ambavyo uwapo wa maumivu ni kama ombi la mwili kuhitaji kupumzika ili kupona kabisa.

Unapobainika na wataalam wa tiba za michezo kuwa una majeraha ya mfupa na nyuzi ngumu (tendon na ligaments) fahamu kuwa itachukua muda kupona kabisa na kurudi mchezoni.

Mwanamichezo anahitajika kujifahamu na kujidhibiti binafsi na maumivu yake ikiwamo kujua yanachokozwa na mambo gani, je yanaanzaje wakati wakuanza, katikati au mwishoni baada ya mazoezi/mchezo?

Vyema pia kufahamu kuwa maumivu yanauma unapominywa au yanakuwepo tu yenyewe, je yanasambaa au yanaibukia sehemu nyingine. Kila tabia ya maumivu ya mwili hutoa picha ya chanzo chake na ukubwa wake.

Wataalam wa tiba za afya za michezo huweza kugundua na kutibu maumivu, kuyatathimini madhara yake kiujumla na huku wakitambua mjongeo wa mwili ambao unaweza kuchochea tatizo hilo kuendana na jeraha lilipo katika mwili.

Baadhi ya makocha, viongozi na mashabiki ndio wanakawaida ya kushinikiza wachezaji walio na majeruhi na maumivu kuwapa dawa za maumivu na kuwalazimisha kushiriki mchezo huku wakijua wazi wana majeraha na hawako imara.

Ikumbukwe kuchoma sindano na kunywa dawa za maumivu zinakwenda kuondoa maumivu na kukupa utulivu kwa muda tu na si kukarabati jeraha na kuliponesha kabisa.

Hata pale anapopona mfupa, msuli au tishu zilizojeruhiwa kwa mara nyingine, hatari ya kujeruhiwa mara kwa mara ni kubwa kwani tishu hizo zinapungua uimara kuweza kuhimili michezo na mazoezi.

Kwa nini matumizi holela ya dawa za muamivu ni hatari

Jambo la msingi kabla ya kutumia dawa zozote vizuri kumwona mtaalam wa afya aliye jirani nawe au mjulishe daktari wa timu kuwa una maumivu yeye ndiye atakaye amua.

Dawa za maumivu ziko za aina nyingi na kila moja au kila jamii ya dawa hizo huwa na kazi tofauti. Zipo zakukabiliana na madogo mpaka ya kati na zipo za maumivu ya kati mpaka makali.

Vile vile dawa hizi huwa na maeneo maalum ya mwilini inapokwenda kufanya kazi.

Zipo ambazo ni maalum kwa ajili maumivu ya kichwa tu, ztumbo, misuli ya pembezone mwa mwili na mishipa ya fahamu. Hutokea wachezaji wakapata uraibu/uteja wa kutumia dawa za maumivu kutokana na kutumia mara kwa mara kiholela.

Hufanya hivyo wakidhani ndiyo wanatibu jeraha kumbe ni kukata maumivu tu lakini tatizo lenyewe haliponi kwa dawa hizo

Tabia hii huwakumbuka sana wachezaji wenye maumivu sugu ya viungo vya mwili. Pasipo kujua kuwa kadiri unavyosababisha uungaji wa jeraha kuchelewa na ndivyo pia huchukua siku nyingi kuwa imara kwa asilimia 100%

Dawa zenye kutumika ni jamii ya Ibuprofen ambazo hushusha mlipuko wa kinga ya mwili unaoleta maumivu katika misuli

Ni vizuri kuepuka kucheza ukiwa na maumivu ya jeraha. Zingatia ushauri wa madaktari wa timu na wataalam wengine wa afya na usitumie dawa kiholela