AFCON 2019: CAF yafuta mechi ya Harambee Stars V Sierra Leone

Muktasari:

  • Oktoba 5, mwaka huu, FIFA iliamua kuifungia Sierra Leone kutokana na kitendo cha serikali ya nchi hiyo kuingilia maswala ya michezo kinyume na sheria za soka, baada ya Wizara ya michezo ya Sierra Leone, kumsimamisha kazi Rais wa Shirikisho la soka la nchini hiyo (SLFA), Isha Johansen, kwa kile kilichodaiwa ni kuhusika na vitendo vya kifisadi.

Nairobi, Kenya. Shirikisho la soka barani Afrika (CAF), imefutilia mbali mechi ya Kundi F ya kusaka tiketi ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON2019) kati ya Kenya na Sierra Leone iliyopangwa kufanyika Novemba 18, ugani Moi Kasarani, Jijini Nairobi.

Uamuazi wa CAF ulitolewa jana jioni, siku sita kabla ya mtanange huo, unatokana na wapinzani wa Kenya, Sierra Leone, kukosa sifa ya kucheza mchezo huo kwa sababu bado wanatumikia kifungo cha shirikisho la soka Duniani (FIFA) na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kwa mujibu wa barua ya kamati ya mashindano ya CAF, kwenda kwa shirikisho la soka nchini (FKF), ni kwamba, kwa kuwa Sierra Leone, bado wanatumikia adhabu ya FIFA, mechi ya Novemba 18, kati Kenya na Sierra Leone, imefutwa na uamuzi wa mwisho kuhusu mustakabali wa kundi F, utatolewa hivi karibuni.

 “Kwa kuwa Sierra Leone bado wanatumukia kifungo cha FIFA, tunaomba kuwaarifu kuwa, mchezo wa kufuzu AFCON, kati ya Kenya na Sierra Leone, uliopangwa kuchezwa Novemba 18, hautofanyika tena.

Pia, ieleweke uamuzi wa mwisho kuhusu mustakabali wa kundi utaamuliwa na kamati tendaji ya CAF baadae,” ilisomeka barua hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya CAF, Khaled Nassar

Oktoba 5, mwaka huu, FIFA iliamua kuifungia Sierra Leone kutokana na kitendo cha serikali ya nchi hiyo kuingilia masuala ya michezo kinyume na sheria za soka, baada ya Wizara ya michezo ya Sierra Leone, kumsimamisha kazi Rais wa Shirikisho la soka la nchini hiyo (SLFA), Isha Johansen, kwa kile kilichodaiwa ni kuhusika na vitendo vya kifisadi.

Kabla ya kupewa kifungo hicho, serikali ya taifa hilo la Afrika magharibi, ilipewa onyo ya kuacha kuingilia masuala ya soka na badala yake kutatua migogoro yake na kuachana na masuala ya soka, lakini walikaidia agizo la CAF na FIFA.

Sierra Leone, walijikuta wakikosa mechi mbili ya nyumbani na ugenini dhidi ya Ghana huku mtanange wa wikendi hii nao ukifutwa na hivyo kufuta ndoto za taifa hilo za kupata tiketi ya kwenda AFCON, itakayofanyika mwakani nchini Cameroon.

Kutokana na hali ilivyo sasa, timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, inayonolewa na Mfaransa, Sebastien Migne, inaongoza msimamo wa Kundi F, ikiwa na pointi saba, pointi nne mbele ya Ghana inayoshika nafasi ya pili, na sita zaidi ya Ethiopia inayoshika nafasi ya tatu.