700 kukinukisha Arachuga

Muktasari:

Akhwari alisema wanariadha nyota wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali duniani watashiriki na kukumbushia aliposhiriki Olimpiki kumaliza km 30 kabla ya misuli kumbana na kuchechemea kwa km 12 zilizosalia na kujikuta akimaliza jioni.

WANARIADHA zaidi ya 700 wanatarajia kuonyeshana kazi kwenye mbio za kimataifa za kumuenzi aliyekuwa mwanariadha mashuhuri nchini, John Steven Akhwari zitakazofanyika Juni 9, jijini Arusha.

Mbio hizo zinazofanyika kwa mara ya kwanza zikifahamika kama ‘John Steven Akhwari International Marathon” zitakuwa na kauli mbiu ya kuhimiza kutokukata tamaa ikirejea kitenco alichokifanya mkongwe huyo alipowakilisha nchi katika Olimpiki za Mexico mwaka 1968.

Akhwari alisema wanariadha nyota wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali duniani watashiriki na kukumbushia aliposhiriki Olimpiki kumaliza km 30 kabla ya misuli kumbana na kuchechemea kwa km 12 zilizosalia na kujikuta akimaliza jioni.

“Watu waliniuliza kwa nini sikuacha kukimbia, lakini nikawajibu: “Nchi yangu haikunituma kuanza bali kumaliza mbio,” alisema mwanariadha huyo mkongwe mwenye miaka 81 sasa.

Mratibu wa mbio hizo, Silvesta Urao amesema hadi sasa maandalizi yamekamilika ikiwemo zawadi na medali mbalimbali huku usajili ukifanyika kwenye ofisi zao katika Mikoa ya Dar es Salaam, Moshi, Mwanza, Tanga na Arusha katika Viwanja vya Sheikh Amri Abeid.

“Mbio hizi zitakuwa na umbali wa kilomita 21. 5 na mbili na nusu ambapo zawadi kwa mshindi wa kwanza ni Sh 800,000, wanaofuata ni Sh 600,000, Sh 450,000, Sh 250,000, Sh200,000 hadi Sh 150,000.”