3.8 Bilioni zatengwa Afcon ya vijana

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Liunda, bajeti hiyo haihusiani na ile ya maandalizi ya timu ya vijana itakayoiwakilisha nchi katika fainali hizo ya Serengeti Boys.


Zikiwa zimesalia siku 30 kabla ya pazia la mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana (Afcon U17) kuanza, Katibu mkuu wa kamati ya Ndani ya maandalizi ya mashindano, Leslie Liunda ametaja bajeti nzima itakayotumika kufanikisha mashindano hayo.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika jana ofisi kwake, jijini Dar es Salaam, Liunda anasema mashindano hayo yametengewa kitita cha Sh 3.8 Bilioni.

Anasema awali bajeti ilikuwa Sh 5.6 Bilioni lakini imepunguzwa na kusalia kitita hicho.

Kwa mujibu wa Liunda, bajeti hiyo haihusiani na ile ya maandalizi ya timu ya vijana itakayoiwakilisha nchi katika fainali hizo ya Serengeti Boys.

“Serengeti yenyewe katika maandalizi yao bajeti yake ni Sh 1.6, bahati nzuri TFF (Shirikisho la Soka) wamesema bajeti hiyo ibaki kwao, na Serikali ibaki na ile ya mashindano ya Sh 3.8 Bilioni,” anasema Liunda.

Anasema nchi inapoandaa mashindano, inayoandaa sio Shirikisho la Mpira bali ni Serikali na hata Malinzi (Jamal rais wa TFF aliyepita) alipoomba Tanzania iwe mwenyeji wa mashindano hayo, aliiuliza Serikali, ikampa ruhusa ya kuomba.

“Kitu kilichomleta Hamad nchini alikuja kusaini makubaliano na Serikali juu ya makubaliano ya kuandaa mashindano kwani TFF haiwezi kuwa na hiyo fedha zaidi ya Serikali.

“Bahati nzuri Waziri Mkuu ametuhakikishia mashindano yatafanyika, Serikali kwa namna ijuavyo kwa kushirikiana na wadau na namna ambavyo Serikali inajiendesha itahakikisha mashindano haya yanafanyika kwa kauli ya Waziri Mkuu” anasema Liunda. Anasema bado wanafungua milango ya udhamini kwa wadau wengine nchini, japo Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeipa Kampuni ya Lagardere mamlaka ya matangazo, lakini atakayehitaji anaweza kwenda kwao na wao wakawapeleka kwenye kampuni hiyo na CAF watakuwa wanajua, lakini pia wanaweza kushirikiana kama ‘patnership’, hiyo inawezekana.

Maandalizi ya viwanja

Liunda anasema viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya mechi ni Uwanja wa

Taifa na Chamazi Complex, huku vile vya mazoezi vikiwa vya JK Youth Park,

Uhuru, Gymkhana, Uwanja wa Chamazi (upo pembeni ya uwanja wa mkubwa wa Chamazi) na Uwanja wa Shule ya Kimataifa ya Hopac.

Tayari Uwanja wa Taifa umeanza kufanyiwa marekebisho, baada ya mechi ya Simba na Vita na ile ya Taifa Stars na Uganda, uwanja huo hautatumika tena hadi kwenye Afcon ya vijana.

“Uwanja wa Uhuru tulitaka utumike katika mechi, lakini CAF walishauri majukwaa ya kawaida nayo yawekewe viti, kitu ambacho katika bajeti ya ukarabati fedha tuliyopewa haikutosha.

“Fedha hiyo ilitosha kubadili kapeti la uwanja, kazi inayoendelea kwa sasa Uwanja wa Uhuru,” anasema Liunda.

Anasema maboresho katika viwanja vyote yanaendelea ambapo viwanja hivyo vitaboreshwa kwa kiwango bora huku Azam wakiukarabati uwanja wao wenyewe, ikiwamo viwanja vitakavyotumika kwa mechi kuwa na vyumba maalumu vya kupimia doping.