19 akiwemo Haji Manara waachiwa kwa dhamana tukio la kutekwa Mo Dewji

Muktasari:

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara ni miongoni mwa watu 19 walioachiwa kwa dhamana jana usiku baada ya kushikiliwa na polisi kwa takribani siku nne wakihusishwa na tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’

Dar es Salaam. Watu 19 kati ya 26 waliokuwa wakishikiliwa na  polisi wakihusishwa na tukio la kutekwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ wameachiwa kwa dhamana jana usiku Oktoba 15, 2018.

Miongoni mwa walioachiwa ni Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara aliyekamatwa Oktoba 12, 2018 kutokana na kusambaza taarifa za tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii kwa madai ya kutumwa na familia jambo ambalo si kweli.

Kauli ya kuachiwa kwa watu hao imetolewa leo Jumanne Oktoba 16, 2018 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

Mambosasa amesema kufuatia kuachiwa kwa watu hao, polisi inaendelea kuwashikilia wengine saba. Hadi jana mchana watu 26 waliokuwa wakishikiliwa na polisi.

Jana,  familia ya Dewji ambaye miaka mitatu iliyopita jarida la Forbes lilimtaja kuwa tajiri namba moja Afrika kwa vijana walio chini ya miaka 40, ilitangaza dau la Sh1bilioni kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwake.

Dewji alitekwa na watu wasiojulikana Alhamisi Oktoba 11, 2018 saa 11:30 alfajiri wakati akiwa Hoteli ya Colosseum na hadi leo saa 3:45 asubuhi hakuna taarifa zozote za watekaji, lengo la kumteka wala fununu za alikohifadhiwa.