HISIA ZANGU: Huyu Manula anasimangwa lakini bado ni tegemeo Simba

AISHI Manula katika lango la Simba amekumbana na misukosuko mingi. Huwa anapatia mara tisa halafu anakosea mara moja. Hiyo mara moja anayokosea wakati mwingine Simba inagharamika kwa matokeo. Mara nyingine timu inashinda halafu anasamehewa.

Majuzi nimemuona akifanya kosa ambalo liliigharimu Simba. Ilikuwa ni bahati mbaya kwamba Simba iliishia kupoteza pambano dhidi ya Prisons. Ilipigwa krosi kutoka upande wa kulia wa Tanzania Prisons na Manula akajaribu kutoka langoni kwake.

Katikati ya safari yake ya kutoka akaghairi na kurudi langoni. Wakati anarudi lango tayari straika wa Prisons, Samson Mbagula alikuwa amepiga kichwa kizito ambacho kilikwenda katika nyavu za Manula na kuiandikia timu yake bao la ushindi.

Baadaye Simba ilinyimwa penalti mbili. Kama ingepewa huenda ingeshinda 2-1 na tusingesikia kelele zozote kuhusu Manula. Bahati mbaya, hata mara ya mwisho wakati Manula alipotunguliwa bao la mbali na Mapinduzi Balama wa Yanga na pambano lao kumalizika 2-2 watu wa Simba walimvaa mzima mzima kwamba, amefungisha.

Sikuwa na tatizo na bao la Mapinduzi, lakini nina matatizo na bao la Mbagula. Kwanini Manula alitoka na kurudi? Sio ugonjwa wake tu, ni ugonjwa wa makipa wengi. Kwa wenzetu kipa akitoka basi ametoka. Akibaki basi amebaki.

Kama Manula angeendelea na safari yake na kuwahi kuugusa mpira kidogo tu basi ule mpira usingetua katika kichwa cha Mbagula. Angeugusa walau kwa kidole tu. Labda aliogopa ajali ambayo ingetokea kati yake, Mbagula na Joash Onyango.

Inawezekana pia wakati akiwa safarini alipima na kugundua kuwa, asingeufikia mpira ndio maana akaamua kurudi. Inashauriwa kwamba ni bora angepima uwezekano huo akiwa amesimama pale pale langoni mwake. Na kama angeamua kutosafiri kuufuata mpira kisha akasimama pale pale basi kichwa cha Mbagula kingeokolewa kwa urahisi.

Nini kinamtokea Manula? Kuna mambo mengi. Jambo la kwanza nina wasiwasi na makocha wa makipa wa timu zetu. Hapa Tanzania tunamchukulia kocha wa makipa kama kocha wa kawaida tu, ambaye hana mchango katika timu. Wenzetu kocha wa makipa anapaswa kuwa na taaluma ya ufundishaji.

Huku kwetu makipa wa zamani wanapewa kibarua hiki kwa sababu tu ya umahiri wao wa zamani. Hatujali sana kama ana uwezo wa kufundisha. Ili mradi alikuwa kipa mzuri basi anapewa kazi hii. Ni vitu viwili tofauti, kuwa kipa mzuri wa zamani na kuwa kocha wa makipa. Hii kazi ya ukocha wa makipa ni taaluma mpya.

Kina Manula inabidi wasaidiwe na makocha wa makipa wenye taaluma za hali ya juu. Kazi ya ukocha wa makipa iheshimiwe kiasi kwamba kipa inabidi aonekane anabadilika kutokana na uwezo wa kocha wake na sio juhudi zake binafsi au kipaji pekee.

Kitu kingine ambacho inawezekana kinamgharimu Manula ni ukosefu wa changamoto katika lango la Simba. Kuna ukosefu wa aina mbili. Kwanza kabisa ana uhakika na nafasi yake. Wakati alipofungwa bao la mbali na Balama nafasi ilikwenda kwa muda kwa Beno Kakolanya.

Bahati mbaya Kakolanya hakuonyesha kiwango chochote cha ajabu cha kuwafanya watu wa Simba wamsahau Manula. Kila mechi aliruhusu mabao rahisi. Manula aliporudi katika lango huu ulikuwa mwisho wa upinzani baina yake na Kakolanya katika lango la Simba.

Pia Manula ameendelea kuwa salama Simba kwa sababu timu yake haina nia ya dhati ya kusaka kipa mwingine wa kuwa namba moja kwa sasa. Kuna sababu mbili. Kwanza ni kwamba hakuna makipa wengi wazuri kwa sasa.

Zamani ingekuwa rahisi tu kwa Simba kuhamia kwingine. Kulikuwa na makipa wengi wenye ubora na pia warefu. Machaguo yalikuwa mengi. Kwa wakati mmoja tumewahi kuwa na Mohamed Mwameja, Joseph Katuba, Steven Nemes, Paul Rwechungura, Madata Lubigisa, Hamis Makene, Riffat Said, Ramadhan Korosheni, Mohammed Nyalusi, Salim Wazir, Kichochi Lemba na wengineo.

Kwa sasa kila ukijaribu kumdharau Manula unajiuliza badala yake utakwenda kwa nani? Jibu linakosekana na unalazimika kuendelea kumheshimu Manula. Hata katika timu ya Taifa, Manula anapewa upinzani na kipa ambaye ni kaka yake wa umri mkubwa, Juma Kaseja na kidogo kwa sasa kwa David Kissu aliyerejea nchini kutoka Gor Mahia ya Kenya.

Kitu kingine ambacho kinafanya maisha kwa Manula yaendelee ni ukweli kwamba hata Simba wenyewe wameamua kuendelea kuwa naye kwa sababu wanajali zaidi nafasi za ndani katika zile nafasi 10 walizopewa kusajili wachezaji wa kigeni.

Klabu nyingi duniani zimekuwa zikihaha kusaka makipa kutoka nchi za nje kutokana na tatizo la makipa ambalo linaendelea kuzisumbua. Angalia katika Ligi Kuu ya England. Kipa wa Manchester United anatoka Hispania, yule wa Arsenal anatoka Ujerumani, huku makipa wa Manchester City na Liverpool wanatoka Brazil, pale Chelsea wao wanaye anayetoka Hispania na sasa wamechukua mwingine kutoka Senegal.

Hata pale Afrika Kusini kina Denis Onyango wameendelea kutesa katika klabu kubwa kwa sababu ya uhaba wa makipa ambao, umeendelea kuwepo nchini humo. Nasi Tanzania tunakabiliwa na ugonjwa huu.

Kwa staili hii tutaendelea kumkashfu Manula huku angali tunamtegemea. Hatuzalishi makipa wa maana tena. Hatuna makocha wa makipa wa uhakika. Lakini hapo hapo wakubwa wetu pia wameamua kuwakumbatia makipa wetu, ingawa nao wanatuangusha kwa kiasi kikubwa wanapokuwa uwanjani ila hatuna cha kufanya sasa.