Azam apanga kumaliza ufalme Simba SC, Yanga

Dar es Salaam. Kocha msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati amesema wanataka kukomesha utawala wa Simba na Yanga zinazopokezana mara kwa mara kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Bahati alisema wamepania ndiyo maana wanapambana kushinda kila mchezo ili kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Azam imeweka rekodi mpya baada ya miaka 12 ya kushinda michezo saba mfululizo msimu huu tangu ilipopanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara 2008.

Kichapo cha mabao 2-0 walichoipa Ihefu juzi kimeifanya Azam kushinda mechi zote saba ilizocheza hadi sasa, jambo ambalo hawajawahi kulifanya tangu walipoanza kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2008/09.

“Msimu huu tumejiwekea malengo na hadi tuyatimize ndio maana unaona kila mchezaji anapambana kuhakikisha kuwa tunatimiza lile tunalolikusudia.

“Azam imetwaa ubingwa mara moja msimu wa 2013/14, hadi sasa haijawahi kufanya hivyo na mara kwa mara tumezoea Simba na Yanga zikipokezana ubingwa.

“Tunakata tubadilishe historia ya hizo timu, tunamaini kutokana na ubora wa kikosi chetu na jinsi wachezaji wanavyopambana naamini Mungu atatusaidia tutafanikisha,” alisema.

Rekodi

Azam ilianza msimu wa 2008/09 kwa kucheza mechi saba, kushinda tatu, sare mchezo mmoja na kupoteza mitatu na msimu uliofuata katika mechi saba ilizocheza ilishinda nne, ikitoka sare miwili na kupoteza mmoja.

Msimu wa 2010/11 ilicheza mechi saba na kupata ushindi katika mechi tatu, ikipoteza tatu na kutoa sare mchezo mmoja na msimu uliofuata, katika mechi saba za mwanzo wa ilishinda nne, sare mbili na kupoteza mmoja.