Kisiga atoa neno kwa mastaa wa kigeni

Muktasari:

Wachezaji wazawa kucheza muda mrefu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, inadaiwa kuwachosha mashabiki wao, kama anavyoelezea kiungo wa Ruvu Shooting, Shaban Kisiga.

KIUNGO wa Ruvu Shooting, Shaban Kisiga amesema kuna changamoto ya kuchokwa na mashabiki kwa wachezaji waliopo muda mrefu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, jambo analoona linazima ndoto za wengi.

Kisiga ametolea mfano wa kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Haruna Moshi 'Boban' kwamba kuna wachezaji wa kigeni wazee kuliko yeye, lakini jinsi ambavyo anachukuliwa na mashabiki anaonekana mkongwe ambaye hawezi kufanya lolote, wakati anaona bado ana uwezo wa kushindana.

Kisiga ameliambia Mwanaspoti, leo Jumatatu Oktoba 19, 2020 kwamba wachezaji wengi wenye vipaji vikubwa wameamua kuzama kucheza ligi ya madaraja ya chini, wanayoamini hakuna mtu ambaye anaweza kuwabeza viwango vyao.

"Nilichokiona mashabiki ama wadau wakimuona mchezaji muda mrefu machoni kwao, wanamchukulia mzee, wakati huo huo angalia wanaowasajili kutoka nje ni wazee kuliko hata wanaowakataa," amesema Kisiga

Ameongeza kuwa "Ni bora wajifunze kupenda vyakwao, kuliko kuchukua wachezaji wa nje ambao wanakuja kustafu hapa nyumbani, wakati mwingine uwezo wao hauwezi kuwashinda wazawa, lakini kwasababu wageni basi wanawasifia kila kona,"amesema.

Kisiga amesema mbali na Boban, amemtaja Kelvin Yondani na Erasto Nyoni kwamba bado anawaona ni watu muhimu kwenye timu ya Taifa Stars, lakini anavyoona mashabiki wamechoka kuwaona.

"Kama Yondani bado naamini ana uwezo mkubwa wakucheza soka la ushindani hata Yanga ambako wamemuacha, Nyoni hivyo hivyo, lakini kwasababu ya maisha yetu Watanzania thamani yao inaanza kushushwa taratibu," amesema.