Solskajaer anatoboa, hatoboi

MANCHESTER, ENGLAND. OLE Gunnar Solskjaer kijasho kinamtoka. Hakuna ubishi, ndiye kocha pekee wa klabu za Big Six mwenye presha kubwa kwenye Ligi Kuu England kwa sasa. Kocha huyo, kwenye mechi tatu za ligi ilizocheza klabu yake ya Manchester United, imeshinda moja tu kwa mbinde - tena dhidi ya Brighton huku ikiruhusu wavu wake kuguswa mara 11 kwenye mechi hizo.

Kwenye mechi tatu ilizocheza Man United, Solskjaer ameshuhudia timu yake ikichapwa 3-1 na Crystal Palace na 6-1 na Tottenham Hotspur wakati mechi iliyoshinda ni dhidi ya Brighton ilikuwa 3-2.

Mapumziko ya mechi za kimataifa pengine yalimpa ahueni kocha Solskjaer, lakini kwa kuanzia wikiendi hii shughuli inarudi huku ikiripotiwa matokeo tu ndicho kitu kitakachookoa ajira yake huko Old Trafford.

Solskjaer shughuli anayo kutokana na ratiba ngumu inayoikabili timu yake, wakilazimika kucheza mechi saba za kibabe ndani ya wiki tatu kwa kuanzia wikiendi hii. Kwenye karatasi mechi hizo zinaweza zisionekane tishio kwa hadhi ya Man United, lakini shughuli ipo ndani ya uwanja, hicho ndicho kinachotishia ajira ya Solskjaer hasa baada ya timu yake kuchapwa mara mbili kwenye mechi tatu.

Man United imepigwa uwanjani Old Trafford mechi mbili mfululizo Ligi Kuu, huku ikiruhusu mabao tisa. Wikiendi hii itakuwa ugenini kwa Newcastle United.

Baada ya hapo, watakwenda ugenini Paris kukabiliana na PSG kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Baada ya hapo, watarudi Old Trafford kukipiga na Chelsea, kisha na RB Leipzig na Arsenal huko Old Trafford.

Baada ya hapo watakwenda ugenini kwa Istanbul Basaksehir kukabiliana na mastaa wa nguvu kama Demba Ba, Nacer Chadli, Martin Skrtel na Rafael da Silva, huku mabingwa hao wa Uturuki wakiripotiwa kuwa kwenye kiwango bora kabisa.

Kisha, wiki ya tatu, Solskjaer atakwenda kuwakabili Everton huko Goodison Park akiwa na shughuli pevu ya kumkabili kocha mwenye uzoefu mkubwa Carlo Ancelotti, ambaye timu yake hiyo imekuwa moto kwelikweli ikiwa na huduma ya James Rodriguez.