Lyanga akipigia mahesabu kiatu cha dhahabu

Muktasari:

Anachokifikiria kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Ayubu Lyanga ni kupambana kuhakikisha anapata nafasi ya kufunga mabao mengi yatakayomuweka kwenye tano bora kwa msimu huu.

 

KIUNGO wa Azam FC, Ayoub Lyanga amesema pamoja na kujituma kwa bidii katika kazi zake, lakini  ushauri wa kaka yake Danny Lyanga  umechangia kwa kiasi kikubwa yeye kufikia hatua aliopo.

 

Amesema kutokana na juhudi ambazo kaka yake alikuwa anazifanya tangu wanakuwa zilimfumbua macho kujua soka bila kupambana ni ngumu kufika mbali.

 

"Danny ni mpambanaji na amenitangulia katika kazi hii, anazijua changamoto za kila aina kwenye soka, jambo ambalo lilikuwa rahisi yeye kunionyesha njia kwamba hiki fanya kile achana nacho,"amesema na ameongeza kuwa.

 

"Kwa kifupi sisi ni zaidi ya kaka na mdogo wake, tumekuwa  marafiki, imefikia hatua yeye anaangalia mechi ninazocheza na yeye naangalia mechi anazocheza, kisha tunaanza kukosoana ana kupongezana, hivyo hakuna anayelala mpaka sasa, ingawa yeye ndiye amekuwa kioo changu,"amesema.

 

Mbali na hilo amezungumzia maisha yake ndani ya kikosi cha Azam, kwamba alipokuwa anajiunga nao, kitu kikubwa alichokuwa anakitamani kifanyike nikupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza.

 

"Tayari ninacheza, hivyo ninachokipigania kwasasa nikuhakikisha napambana kufunga mabao mengi ili kuwa kwenye kinyang'anyiro cha wale ambao watakuwa kwenye tano bora, hilo linawezekana ndio maana nafanya bidii,"amesema.

 Lyanga  amejiunga na Azam FC, msimu huu akitokea Coastal Union ya Tanga, jambo ambalo amesema linamfanya ajitume ili timu ifaidike na huduma yake