Soko baya, masupastaa wa nguvu ambao thamani zao sokoni zimeshuka

LONDON, ENGLAND. MSIMU mpya wa 2020/21 umeanza kushika kasi na Jumatatu iliyopita ulikuwa mwisho wa usajili wa wachezaji huko kwenye soka la Ulaya.

Janga la corona lilitawala biashara za usajili wa wachezaji kwenye dirisha hilo lililomalizika la majira ya kiangazi licha ya klabu kama Chelsea kuonyesha jeuri ya matumizi ya pesa wakati ilipowanasa Timo Werner, Kai Havertz na Hakim Ziyech kwa pesa ndefu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Transfermarkt, thamani za wachezaji wengi huko Ulaya zimeshuka sana kiasi cha kutisha, huku supastaa Eden Hazard akiporomoka kwa zaidi ya Pauni 50 milioni.

Kutokana na hilo, hii hapa orodha ya masupastaa 20, ambao thamani zao sokoni zimeshuka kwa kiwango kikubwa kwa mujibu wa Transfermarkt.

20.Luis

Suarez (Atletico)

Imeshuka: Pauni 19.8 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 16.2 milioni

Baada ya kufunkufunguliwa mlango wa kutokea huko Barcelona, straika Luis Suarez ametumikia Atletico Madrid, mahali ambako amenaswa kwa ada isiyozidi Pauni 5 milioni. Umri na janga la corona limedaiwa kushusha thamani ya mshambuliaji huyo kwa Pauni 19.8 milioni na kumfanya awe na thamani ya Pauni 16.2 milioni kwa sasa.

19.Alexandre Lacazette (Arsenal)

Imeshuka: Pauni 19.8 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 43.2 milioni

Straika, Alexandre Lacazette ni mmoja wa wachezaji ambao thamani zao zimeshuka huko sokoni kwa Pauni 19.8 milioni na hivyo kwa sasa kuthaminishwa kwa thamani ya Pauni 43.2 milioni. Kilichoshusha thamani ya Mfaransa huyo ni ubora wake wa ndani ya uwanja licha ya sasa ameanza kurudi kwa kasi akiwa amefunga mabao matatu katika mechi nne.

18.Lucas Hernandez (Bayern Munich)

Imeshuka: Pauni 22.5 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 40.5 milioni

Majeruhi yametibulia sana beki, Lucas Hernandez maisha yake huko kwenye kikosi cha kwanza cha Bayern Munich. Jambo hilo limeathiri hadi thamani yake ya sokoni, ikishuka kwa Pauni 22.5 milioni na hivyo kumfanya mkali huyo wa Ufaransa kuwa na thamani ya Pauni 40.5 milioni. Herndandez bado yupo kwenye orodha ya mabeki wa kiwango cha dunia.

17.Ousmane Dembele

(Barcelona)

Imeshuka: Pauni 22.5 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 45 milioni

Staa mwingine, ambaye thamani yake sokoni imeshushwa kutokana na kusumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara. Dembele ameshindwa kuitumikia Barcelona kwa muda mrefu, mara chache alizoonekana uwanjani alijaribu kuonyesha ubora wake, lakini majeruhi yametibua na kushusha thamani yake ya sokoni kwa Pauni 22.5 milioni.

16.Dele Alli

(Tottenham)

Imeshuka: Pauni 23.4 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 57.6 milioni

Ukweli ni lazima usemwe, kiwango cha Dele Alli kimeshuka kwa kasi kubwa tangu alipokuwa moto kabisa katika msimu wa 2016/17. Staa huyo kwa sasa amekuwa kwenye wakati mgumu huko Tottenham Hotspur baada ya kutokuwa kwenye uhusiano mzuri na kocha wake Jose Mourinho. Kuporomoka kiwango chake kimeporomosha pia thamani yake sokoni kwa Pauni 23.4 milioni.

15.Sergi Roberto

(Barcelona)

Imeshika: Pauni 27 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 18 milioni

Staa wa Barcelona, Sergi Roberto ni miongoni mwa wachezaji ambao thamani zao zimeshuka sokoni, ambapo imeporomoka kwa Pauni 27 milioni na kumfanya thamani yake ya sokoni kwa sasa kuwa Pauni 18 milioni pekee. Anapokuwa kwenye ubora wake, Sergi Roberto anakuwa moto kwelikweli, lakini kucheza chini ya kiwango kumeporomosha pia thamani yake sokoni kwa kiasi kikubwa.

13.John Stones (Man City)

Imeshuka: Pauni 27 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 27 milioni

Beki wa kati wa Manchester City, John Stones mambo yake si mazuri kabisa kutokana na thamani yake sokoni kushuka kwa nusu nzima. Mwingereza huyo thamani yake imeshuka kwa Pauni 27 milioni na hivyo thamani yake ya sokoni kwa sasa ni Pauni 27 milioni. Kutokana na kocha Pep Guardiola kuwekeza kwenye usajili wa mabeki wapya hilo linadhihirisha hana chake tena.

12.Christian Eriksen

(Inter Milan)

Imeshuka: Pauni 27 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 54 milioni

Kuna wakati, kiungo Christian Eriksen alipokuwa Tottenham Hotspur, saini yake kuipata ilikuwa lazima iwe ndefu. Lakini, Spurs ilijichelewesha kumwongeza dili jipya na kulazimisha kumuuza kwenda Inter Milan kwa bei ya chini. Baada ya kutua Italia, maisha ya Eriksen yalibadilika na kiwango chake kushuka na kusababisha thamani yake sokoni kushuka kwa Pauni 27 milioni.

11.Leroy Sane (Bayern Munich)

Imeshuka: Pauni 27 milioni

Thamani ya sasa:

Pauni 63 milioni

Manchester City iligoma sana kumwaachia staa wake, Leroy Sane kwa pesa kiduchu, lakini majeruhi yaliwalazimu kukubali aende Bayern Munich licha ya haikuwa kwa pesa waliyokuwa wanataka kumuuza. Staa huyo wa kimataifa wa Ujerumani, thamani yake sokoni imeshuka kwa Pauni 27 milioni.

10.Sadio Mane (Liverpool)

Imeshuka: Pauni 27 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 108 milioni

Licha ya kuwapo kwa janga la virusi vya corona, thamani ya supastaa wa Liverpool, Sadio Mane haijashuka kiwango cha kutisha huko sokoni, bado huwezi kunasa saini yake kwa mkwanja usiopungua Pauni 108 milioni. Hata hivyo, Mane angeuzwa kwa pesa nyingi zaidi kama si thamani yake hiyo sokoni kushuka kwa Pauni 27 milioni.

9.Harry Kane

(Tottenham)

Imeshuka: Pauni 27 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 108 milioni

Kama ilivyo kwa Sadio Mane, straika Harry Kane naye thamani yake sokoni imeshuka kwa Pauni 27 milioni. Hata hivyo, thamani yake ya sasa, huwezi kupata huduma yake bila ya kuweka mezani mkwanja unaozidi Pauni 100 milioni. Kane amekuwa kwenye kiwango bora katika Ligi Kuu England msimu huu, ambapo tayari ameshahusika kwenye asisti saba kwenye ligi hiyo msimu wa 2020/21.

8.Mo Salah (Liverpool)

Imeshuka: Pauni 27 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 108 milioni

Mkali mwingine kwenye kikosi cha Liverpool, ambaye thamani yake sokoni haikuathiriwa sana na COVIC 19 licha ya kwamba imeshuka kwa thamani kubwa sana. Mohamed Salah, thamani yake sokoni imeshuka kwa Pauni 27 milioni, lakini kupata huduma yake itakulazimu utoe mkwanja mrefu, si pungufu ya Pauni 108 milioni kulingana na thamani yake ya sokoni kwa sasa.

7.Kevin De Bruyne

(Man City)

Imeshuka: Pauni 27 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 108 milioni

Ndio, kwa thamani ya Kevin de Bruyne kwa sasa huko sokoni ni Pauni 108 milioni. Kama isingekuwa janga la virusi vya corona, mchezaji huyo angeuzwa kwa dai kubwa zaidi kwa kuzingatia thamani yake baada ya kuripotiwa kwamba imeshuka kwa Pauni 27 milioni. De Bruyne ni moja ya wachezaji ambao hakuna kocha wa klabu kubwa za Ulaya asiyetaka kuwa na huduma yake kwenye kikosi chake.

6.Kepa Arrizabalaga

(Chelsea)

Imeshuka: Pauni 28.8 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 25.2 milioni

Kipa, Kepa kwa sasa hana uhakika wa kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha Chelsea baada ya ujio wa kipa mpya, Mendy. Kocha wa miamba hiyo ya Stamford Bridge, Frank Lampard amefanya usajili wa kipa mpya kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa wachezaji baada ya kuchoshwa na huduma ya Kepa. Kiwango kibovu kimemfanya Kepa thamani yake kushuka kwa Pauni 28.8 milioni huko sokoni.

5.Raheem Sterling

(Man City)

Imeshuka: Pauni 28.8 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 115.2 milioni

Raheem Sterling alikuwa kwenye kiwango bora sana kwenye msimu wa 2019/20 na mwingine nyuma yake. Lakini, hapo katikati, winga huyo mfungaji alipoteza uwezo wake wa kutumbukiza mipira wavuni na hivyo jambo hilo limemfanya apoteze ubora wa thamani yake sokoni na kushuka kwa Pauni 28.8 milioni. Hata hivyo, Sterling bado bei yake ipo juu, bila ya Pauni 115.2 milioni hujanasa saini yake.

4.Neymar (PSG)

Imeshuka: Pauni 28.8 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 115.2 milioni

Mwanasoka ghali zaidi kwa sasa kwa maana ya pesa iliyolipwa kunasa saini yake ni Neymar, wakati PSG ilipoilipa Barcelona Pauni 198 milioni kunasa saini yake miaka mitatu iliyopita. Lakini, majeruhi na mambo mengine yamemfanya staa huyo thamani yake kuporomoka kwa Pauni 28.8 milioni na sasa anadaiwa thamani yake ni Pauni 115.2 milioni.

3.Antoine Griezmann

(Barcelona)

Imeshuka: Pauni 36 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 72 milioni

Maisha ya Griezmann baada ya kutua Barcelona akitokea Atletico Madrid yamekuwa tofauti, kiwango chake cha soko kikishuka kwa thamani kubwa kwa Pauni 36 milioni. Kinachoelezwa ni kwamba thamani ya mchezaji huyo sokoni kwa sasa ni Pauni 72 milioni tu, licha ya kutocheza kwa kiwango bora cha soka lake, akiwa amefunga mabao 15 katika mechi 48 katika msimu wake wa kwanza.

2.Lionel Messi

(Barcelona)

Imeshuka: Pauni 36 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 90 milioni

Akifunga zaidi ya mabao 20 na asisti 20 kwa msimu uliopita akiwa kwenye kikosi cha Barcelona, Lionel Messi ubora wake wa uwanjani ulikuwa juu na angeweza kuwa na thamani kubwa kama si mkataba wake kuwa kwenye mwaka wa mwisho, ingekuwa juu zaidi. Messi thamani yake kwa sasa imeshuka kwa Pauni 36 milioni na kumfanya sokoni kwa sasa awe na thamani ya Pauni 90 milioni.

1.Eden Hazard

(Real Madrid)

Imeshuka: Pauni 54 milioni

Thamani ya sasa: Pauni 54 milioni. Mambo yamekuwa magumu sana kwa Eden Hazard tangu alipojiunga na Real Madrid. Staa huyo wa zamani wa Chelsea mdiye mchezaji ambaye thamani yake imeshuka kwa kiwango kikubwa sana, Pauni 54 milioni huku thamani kubwa ikidaiwa kuwa ni majeruhi yaliyomweka nje kwa muda mrefu. Jambo hilo lilishusha pia kiwango cha mchezaji huyo na kuathiri soko lake, ambapo kwa sasa thamani yake ni Pauni 54 milioni.