Kagere, Mugalu wana jambo lao Jangwani

MASTRAIKA Meddie Kagere na Chris Mugalu wamekutana na makali ya Prince Dube katika vita ya kuwania ufungaji bora msimu huu, lakini nao wamegeuzia moto wao kwa Yanga kwa kusepa na kijiji Jangwani kwa kufunga mabao ambao ni idadi sawa na yale yaliyofungwa na kikosi kizima cha wapinzani wao hadi sasa katika ligi.

Licha ya Kagere na Mugalu, kila mmoja kushindwa kumfikia Dube anayeongoza kwa mabao matano kwenye orodha ya Wafungaji wa Ligi Kuu Bara, mastraika hao bado wanacho cha kuwatambia wenzao wa Yanga kwa kuwaacha mbali katika ufungaji kwenye raundi tano za mwanzo.

Kagere na Mugalu sio tu wamewafunika washambuliaji wa Yanga, lakini pia wameonekana kula sahani moja na kikosi kizima cha timu hiyo katika kufumania nyavu.

Katika mechi za raundi tano za mwanzo, Kagere na Mugalu ambao awali walikuwa hawaanzi kikosi cha kwanza cha Simba, wamepachika jumla ya mabao saba katika mechi tano dhidi ya Ihefu, Mtibwa Sugar, Biashara United, Gwambina na JKT Tanzania.

Idadi hiyo ya mabao saba ndio kiujumla imefungwa na Yanga nzima katika mechi zao tano za mwanzo dhidi ya Prisons, Mbeya City, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na Coastal Union.

Kati ya mabao hayo saba ambayo wawili hao wamefunga, manne yamepachikwa na Kagere katika mechi dhidi ya Gwambina, Biashara na JKT, huku akishindwa kufunga katika michezo miwili dhidi ya Mtibwa na Ihefu.

Kwa upande wa Mugalu amefunga mabao matatu katika mechi tatu tu za ligi alizoichezea timu hiyo dhidi ya Gwambina, Biashara na JKT, akipachika bao moja katika kila mechi.

Kana kwamba haitoshi mabao yao saba waliyofunga ni mara mbili zaidi ya mabao yaliyofungwa na washambuliaji wawili wa Yanga, Yacouba Songne na Michael Sarpong ambao wamefumania nyavu mara mbili, moja kwa kila mchezaji.

Sarpong alifunga bao lake moja pekee katika mechi ya Yanga dhidi ya Prisons iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 huku Yacouba akipachika bao lake katika mchezo dhidi ya Coastal Union ambao waliibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Mabao mengine ya Yanga yamefungwa na wachezaji wanaocheza katika safu ya kiungo na beki ambapo kwa nafasi ya viungo waliofunga ni Tonombe Mukoko, Carlos Carlinhos na Haruna Niyonzima, huku mawili yakiwekwa wavuni na beki wa kati Lamine Moro, akiwa ndiye kinara wa mabao Jangwani.

Juu ya kasi ya nyota wa Simba, Kocha wa Biashara United, Francis Baraza alisema kuwa Simba inabebwa zaidi na ubora wa wachezaji wake hasa wa safu ya kiungo.

“Daraja la wachezaji wa Simba ni tofauti na wa timu nyingi. Wana wachezaji wazuri wanaoweza kutengeneza nafasi na kukuadhibu pale unapofanya makosa hivyo sio rahisi kucheza nao,” alisema Baraza.

Kocha wa Pamba na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe alisema kuwa aina ya soka wanalocheza Simba ndio siri ya mafanikio ya washambuliaji wake.

“Simba ni timu inayocheza soka la pasi na inayocheza kwa nafasi hivyo inakuwa rahisi kwa washambuliaji wake kupata huduma nzuri na kufunga mabao lakini bado lazima tusifu ubora wao wenyewe katika kufunga.

“Binafsi naamini sio kazi rahisi kucheza dhidi ya Simba ikiwa katika ubora wake na inaweza kukufunga nyingi,” alisema Mwakingwe.