Deal done, sajili matata za D-Day ligi kuu England, Ole apumua Man Utd

LONDON, ENGLAND. NANI imekula kwao? Kocha wa Chelsea, Frank Lampard ni kama mambo yake alimaliza mapema kwenye dirisha la usajili kwa kunasa mastaa wapya kibao.

Hata hivyo, wakati anaingia siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha hilo la uhamisho wa majira ya kiangazi jana Jumatatu, Lampard alikuwa na huduma moja anayofukuzia, alikuwa akisaka kiungo mkabaji.

Kwa siku hiyo ya jana, Manchester United ilikuwa bize kusaka huduma za wachezaji kadhaa ikikimbizana na muda kama ilivyokuwa kwa Arsenal, Manchester City na Tottenham Hotspur.

Ripoti zinadai Man United ilikuwa sokoni ikijaribu kusaka wachezaji watatu kwenye siku ya mwisho kabla ya dirisha kufungwa, huku kocha wa Arsenal, Mikel Arteta alipewa uhakika mkubwa wa mabosi wake kwamba kuna uwezekano mkubwa akanaswa staa mpya kabla ya muda wa usajili wa dirisha hili la majira ya kiangazi kupita.

Edinson Cavani na Alex Telles ni moja ya wachezaji walioripotiwa kuwa kwenye hatua za mwisho za kutua huko Old Trafford kwenda kukipiga chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer, lakini mpango wa timu hiyo kwa siku ya jana ilikuwa pia kunasa huduma ya winga mmoja kati ya Ousmane Dembele na Jadon Sancho.

Hizi hapa dili 10 kati ya kibao zilizokuwa zikisubiriwa kwa hamu kubwa kukamilika kabla ya dirisha la usajili kufungwa jana Jumatatu. Je, zimetiki?

10. Xherdan Shaqiri

Liverpool ilionekana kama vile imeshamalizana na wachezaji wapya wa kutua kwenye kikosi chao, lakini kocha Jurgen Klopp alifungua milango ya Shaqiri kuondoka kwenye kikosi hicho. Wakati jana Jumatatu ikiwa ni siku ya mwisho ya usajili, Sevilla na Lazio zilikuwa zikichuana vikali kusaka huduma ya staa huyo wa kimataifa wa Uswisi ikiwa ni moja ya dili zilizokuwa zikisubiriwa kukamilika hadi dakika za mwisho.

9. Declan Rice

Kocha wa Chelsea, Frank Lampard alikuwa bize kwenye siku ya mwisho kujaribu kunasa huduma ya kiungo mkabaji, Declan Rice kuimarisha kikosi chake ikiwa ni mwendelezo wa kutupia pesa nyingi kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi. Hata hivyo, shughuli ya kunasa huduma ya Rice ilikuwa pevu hadi dakika za mwisho kabisa kutokana na West Ham United hawakuwa tayari kumuuza mchezaji huyo, hivyo Chelsea ilikuwa ikipambana huku ikitafuta mbadala wake.

8. Thomas Partey

Kiungo mkabaji wa Atletico Madrid, Thomas Partey kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi amekuwa akisakwa na timu za Arsenal na Chelsea na katika siku ya jana ya kufungwa kwa dirisha la usajili, miamba hiyo ya Ligi Kuu England ilichuana jino kwa jino.

Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta kwa muda mrefu alikuwa akisaka saini ya Partey, lakini dakika za mwishoni Chelsea iliingiza mguu wao baada ya kuona ishu ya kumnasa Declan Rice inaweza kushindikana.

7. Edinson Cavani

Manchester United ilikuwa kwenye mchakato wa kuboresha safu yao ya ushambuliaji hivyo, Kocha Ole Gunnar Solskjaer alikuwa kwenye mchakato wa kukamilisha usajili wa straika veterani Edinson Cavani kabla ya dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi kufungwa.

Katika siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili, ishu ya Cavani kwenda Man United ilionekana kukamilika kwenye kila kitu hasa ukizingatia mchezaji mwenye ni huru baada ya kumalizana na PSG.

6. Lucas Torreira

Hili ni dili lililotarajia kuwashangaza wengi lingekamilika katika siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili. Kiungo huyo wa kimataifa wa Uruguay, aliripotiwa aliingia siku ya mwisho ya kufungwa kwa usajili akiwa tayari ameshapima vipimo vya afya na kukubaliana mambo binafsi na klabu ya Atletico Madrid.

Hata hivyo, shida ilikuwa sehemu moja tu, Atletico ilitaka imuuze Hector Herrera kwanza kabla ya kumtangaza Torreria na kila kitu kilisubiriwa siku hiyo.

5. Antonio

Rudiger

Kocha, Frank Lampard amemweka kando beki wa Kijerumani, Antonio Rudiger kwenye mechi tano na jambo hilo lilizifanya klabu za Tottenham Hotspur na Paris Saint-Germain kuanza kufukuzia huduma yake. Mambo yalikuwa mengi kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili, ambapo Chelsea wao walikuwa tayari kufanya biashara ya kumuuza jumla kuliko kutoa kwa mkopo. Dili la Rudiger lilikuwa kwenye mchakato wa kukamilika kwenye siku ya mwisho.

4. Alex Telles

Baada ya kuvumishwa kwa karibu wiki nzima, Manchester United ilionekana kupiga hatua nzuri ya kunasa huduma ya beki Alex Telles kutoka FC Porto hadi ilipofika siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili la majira ya kiangazi huko Ulaya. Mwanzoni, FC Porto iligomea ofa ya Man United, lakini miamba hiyo ya Old Trafford ililazimisha uhamisho huo na ilipambana kwa nguvu zote kukamilisha uhamisho huo kwenye siku ya mwisho ya usajili kabla ya dirisha kufungwa.

3. Dele Alli

Hapo zamani za kale, staa wa Kingereza, Dele Alli alikuwa hawezi kuwekwa benchi kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur, lakini kwa sasa tangu alipotua, Jose Mourinho kila kitu kimebadilika. Paris Saint-Germain imeonyesha dhamira ya dhati ya kunasa huduma ya staa huyo, ikipeleka ofa ya mkopo mara kadhaa na mabosi wa Spurs waliigomea.

Hata hivyo, kila kitu kilisubiriwa kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili, ambapo Dele mwenyewe alihitaji kuondoka.

2. Ousmane Dembele

United matakwa yao ya kutaka winga wa kulia iliwafanya wapige hodi huko Barcelona kwenda kuulizia huduma ya Mfaransa, Ousmane Dembele. Kwa ripoti za kufikia jana ambapo ilikuwa siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili, kocha wa Barcelona, Ronald Koeman aliripotiwa kuwaambia mabosi wa Man United kwenda kumsajili staa huyo kwa mkopo kama wanavyotaka endapo kama itakuwa imekwama kwenye mpango wa kumnasa Jadon Sancho.

1. Jadon

Sancho

Kwa muda wote wa dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi, Jadon Sancho alikuwa akihusishwa na Manchester United na kila kitu kilisubiriwa kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa usajili. Man United ilihitaji kutumia akili kubwa ya kukamilisha dili la Sancho katika siku hiyo ya mwisho, huku bosi Ed Woodward aliripotiwa kuongeza ofa y a kumsajili staa huyo, ambaye klabu yake ya Borussia Dortmund ilihitaji ilipwe Pauni 108 milioni. Dortmund ilidaiwa kukubali kushusha bei ya kumuuza Sancho dakika za mwisho.