Mastaa watatu wafungua akaunti ya mabao Yanga

Muktasari:

Kwa mara ya kwanza tangu msimu huu kuanza kwenye Ligi Kuu Bara, Yanga wamepata ushindi wa mabao 3-0, dhidi ya Coastal Union.

Kwa mara ya kwanza tangu msimu huu kuanza kwenye Ligi Kuu Bara, Yanga wamepata ushindi wa mabao 3-0, dhidi ya Coastal Union.

Matokeo hayo yameifanya Yanga, kuongoza msimamo wa ligi wakiwa wamefikisha pointi 13, huku wakiwa wamefunga mabao saba na wao kufungwa moja katika mechi tano ambazo wamecheza mpaka sasa.

Katika mechi hii dhidi ya Coastal Union, mastaa watatu wa Yanga, walifungua akaunti za mabao msimu huu kila mmoja akifunga bao moja.

Staa wa kwanza kufungua akaunti alikuwa kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo, Carlo Corlinhos aliyefunga bao dakika 48, na baada ya hapo walifuata Haruna Niyonzima dakika 53, na Yacouba Sogne dakika 63.

Mechi hiyo iliyomalizika kipindi cha kwanza bila bao lolote kwa timu zote mbili, ilikuja kubadilishwa kipindi cha pili baada ya kufanyika mabadiliko kwa upande wa vinara Yanga.

Niyonzima aliyochukua nafasi ya Zawadi Mauya aliyecheza kwa dakika 45, aliweza kubadili mpira na Yanga kucheza tofauti na kipindi cha kwanza.

Kiungo huyo fundi, alikuwa akichukua mipira na kuanzisha mashambulizi ambayo yalisababisha safu ya ulinzi ya Coastal Union kufanya makosa mara kwa mara ambayo yakisababisha kufungwa mabao hayo.

Coastal Union baada ya kufungwa waliendelea kucheza kama kipindi cha kwanza walikuwa wakitengeneza mashambulizi ambayo walishindwa kuyatumia.