Belqola mwamuzi wa kihistoria aliyechezesha Kombe la Dunia ‘98

IMETIMIA miaka 90 tangu zilipofanyika fainali za kwanza za soka za Kombe la Dunia nchini Uruguay 1930 na wenyeji kubeba kulinyakua baada ya kuifunga Brazil.

Morocco ilikuwa nchi ya kwanza na pekee ya Afrika kucheza fainali hizo katika mashindano ya pili yaliyofanyika huko Italia 1934.

Nchi hiyo iliyopo Kaskazini Magharibi mwa Afrika pia iliweka rekodi ya kutoa Mwafrika wa kwanza na pekee hadi sasa kuchezesha mchezo wa fainali za mashindano hayo makubwa kabisa duniani.

Mwamuzi huyo ni Said Belqola, aliyepewa jukumu la kuchezesha pambano la kukata na shoka la mchezo wa fainali kati ya Brazil waliopewa nafasi kubwa ya ushindi na wenyeji wa mashindano - Ufaransa mwaka 1998.

Katika mchezo huo ambao Zinedine Zedane aling’ara na mchango wake kuwa sehemu muhimu ya historia ya mashindano hayo kama ilivyo kwa mwamuzi Belqola.

Ufaransa ilibeba ubingwa wa Kombe la Dunia kwa ushindi wa mabao 3-0 ambao uliushangaza ulimwengu.

Shirikisho la Soka duniani (Fifa) lilipomtangaza Belqola kuwa mwamuzi wa mchezo huo wa fainali, wapo wachambuzi wa michezo na waandishi wa habari walioeleza wasiwasi wao kama angehimili vishindo na mikiki ya mchezo mkubwa kama ule.

Lakini, Fifa ilisisitiza kwamba baada ya kufanya tathmini ya waamuzi wote waliokuwepo Ufaransa katika fainali hizo za 1998, ilibaini kuwa hkuna aliyekuwa bora zaidi ya Belqola na ndio maana waliamua kumpa hiyo dhamana.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kama uamuzi ule ulimshangaza na iwapo angeumudu mchezo, Belqola alitabasamu .

Aliwaambia waandishi wa habari: “Nyie ndio mnaoshangaa na sio mimi. Ninaamini nitapata tabu kama sheria za mchezo wa kandanda na kanuni zake zitabadilika au badala ya kuchezesha watu 22 walioingia uwanjani nitakuwa nachezesha ndege au wanyama 22.”

Belqola ambaye alifariki dunia mwaka 2002 kwa ugonjwa wa saratani, alisifika sana kwa namna alivyousimamia vizuri mchezo ule wa fainali kama alivyokuwa katika michezo mingine ya kimataifa na kusababisha kupewa jukumu la kuchezesha fainali hiyo.

Kabla ya kuchezesha michezo ya kugombea tiketi za kufuzu fainali za Kombe la Dunia, Belqola alikuwa mwamuzi wa michezo mbalimbali ya kimataifa nchini kwao Morocco, na katika nchi nyingi za Afrika, Asia na Ulaya.

Mara nyingi kila ulipokuwepo mchezo wa fainali wenye mvutano mkali wa washiriki - iwe klabu au mataifa, katika nchi za Ghuba na Asia, Belqola aliitwa kuwa mwamuzi wa mchezo.

Belqola ambaye umaarufu wake Morocco ni ‘mtoto mtiifu wa Tilfet’ (mji mdogo uliopo Kaskazini mwa Morocco), ni mwamuzi aliyekuwa hana tabia ya kuzungumza na wachezaji uwanjani.

Kila alipochezesha alitumia mikono kujieleza au kadi kwa yeyote ambaye hakuonyesha mchezo mzuri.

Kwa upande wake ilikuwa kawaida mchezaji anapomlalamikia alikuwa anaziba masikio kwa mikono ili asisikie anachoambiwa.

Baada ya masomo ya elimu ya dini na dunia, alifanya kazi kama ofisa wa forodha katika mji wa Fez, Morocco na wakati akikitumikia cheo chake alipachikwa jina la utani na wafanyabiashara kama ‘Bwana wa Sheria’.

Baada ya kuchezesha michezo ya madaraja tofauti nyumbani kwao Morocco ikiwa pamoja na Ligi Kuu alizochezesha katika nchi jirani na mashindano ya klabu na mataifa ya Afrika na Asia.

Alichaguliwa kuwa mwamuzi wa kimataifa mwaka 1993 na mchezo wake mkubwa wa kwanza ulikuwa kusimamia pambano kati ya Ufaransa na England lililofanyika nchini Ufaransa 1997.

Vilevile alikuwa miongoni mwa waamuzi waliochaguliwa kwa fainali za Kombe la Mataifa la Afrika (Afcon) za 1996 na 1998.

Wakati wa fainali za Kombe la Dunia 1998, pia alichezesha mapambano kati ya Ujerumani na Marekani na lile la Argentina na Croatia.

Fifa ilimchagua kuwa mwamuzi bora wa robo ya mwisho wa karne ya 20.

Vilevile alichaguliwa na Chama cha Soka cha Nchi za Kiarabu kuwa mwamuzi bora wa nchi za Kiarabu wa mwaka 1998.

Mwamuzi huyo aliaga dunia akiwa nyumbani kwake katika jiji la Rabat, Morocco mwaka 2002 baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na ugonjwa wa saratani.

Wachezaji na waamuzi wengi mashuhuri duniani walihudhuria mazishi yake.

Mwamuzi mmoja alisema Belqola ameshapuliza filimbi ya mwisho ya maisha yake, lakini sauti ya hiyo filimbi itaendelea kusikika siku zote.

Mchezaji mahiri wa kiungo wa Misri wa miaka ya mwisho ya 1990 hadi mwaka 2013, Mohamed Aboutrika katika salamu zake za rambirambi alisema alimheshimu Belqola kama mmoja wa waamuzi wazuri duniani.

‘’Wakati wowote ule angechaguliwa kutuchezesha Misri na Morocco ningekuwa sina kinyongo. Mapenzi yake yalikuwa kwa sheria za mchezo na sio klabu au mchezaji,’’ alisema.

Katika maelezo ya kumbukumbu zake muhimu kama mwamuzi wa kandanda aliyoyatoa miaka miwili kabla ya kifo chake, Belqola alisema alipata habari kwamba ule mchezo wa fainali kati ya Brazil na Ufaransa ambao aliusimamia kama mwamuzi, wachezaji wa Brazil walitiliwa dawa katika chakula na kuonekana hawana nguvu uwanjani.

“Nilishangazwa sana na namna Brazil walivyocheza. Walionekana wamechoka tangu mwanzo wa mchezo na hii imenisababisha kuamini walichezewa mchezo mchafu nje ya uwanja,” alisema Belqola.

Mwamuzi huyo alisema wachezaji wa Brazil walikuwa hawaelewani hata kidogo, waligombana ovyo na Ronaldo ambaye alikuwa ni mchezaji nyota wa kikosi hicho alikuwa sio mchezaji ambaye mashabiki walimfahamu vyema.